Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewataka Wazazi , walezi, viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa maendeleo kukumbuka jukumu lao la kuwalinda watoto ili kuwajengea ustawi wa kesho kwa kuwaunda kuwa watumishi bora katika Taifa la kesho.
Mhe. Shaka ameyasema hayo Juni 16, 2025 akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa Wilayani Kilosa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kilosa Town ambapo amesema wazazi wanatakiwa kukaa karibu na watoto ili kujua wanayoyapitia na wawe huru kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo viovu.
Sambamba na hayo amewataka Maafisa Maendeleo na Ustawi wa jamii katika ngazi ya Halmashauri na Kata waendelee kuimarisha elimu, malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi na walezi ili waelewe wajibu wao wa kuwalea watoto kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa wa kijinsia.
Aidha Shaka ameongeza kwa kusema kuna ripoti mbalimbali zimeeleza kuwa bado watoto wanakabiliwa na changamoto za vitendo vya ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ubakaji, ulawiti, utumikishwaji katika ajira hatarishi, utekaji, vipigo, kuchomwa moto, mimba za utotoni na ukatili wa mitandaoni ambapo katika kuhakikisha haki za watoto zinalindwa serikali kwa kushirikiana na wadau imefanya jitihada za kuratibu na kusimamia program ya taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto kwa mwaka 2020/ 2025.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Morogoro Gibson Mwakoba amesema maadhimisho hayo yametokana na tukio la Mauaji ya watoto elfu mbili ambalo lilitokea Juni 16, 1976 katika Kitongoji cha Soweto Nchini Afrika Kusini ambapo mauaji hayo yalitokea baada ya watoto hao kuamua kuandamana kudai haki yao ya kutobaguliwa sawasawa na wengine hivyo Jamii na wazazi wote wanapaswa kuhakikisha kuwalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata Wadau mbalimbali wa maendeleo, watoto na wananchi kwa ujumla yakiambatana na kauli mbiu isemayo “HAKI ZA MTOTO ,TULIPOTOKA ,TULIPO NA TUENDAKO”
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa