Watendaji wa kata, vijiji na wenyeviti wa vitongoji wametakiwa kujituma kwa bidiii katika majukumu yao huku wakizingatia miiko ya majukumu ya kuwatumikia wananchi lengo ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto za wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga alipozungumza na watendaji hao ambapo amewataka kazi iwe ndio kipaumbele cha kwanza huku akisisitiza uwepo wa nidhamu kuanzia ngazi ya chini kwa kushirikiana badala ya kutunishiana misuli kwani kila mmoja yupo kisheria kwa majibu wa majukumu yake.
Mwanga ametaka kufanyika kwa mikutano yote ya kisheria ambapo ameagiza wenyeviti wa vitongoji kuanzia Juni 1 hadi 10 kuhakikisha mikutano yote stahiki iwe imeshafanyika huku akitaka mihutasari ya vikao hivyo iwe imefika kwa watendaji wa kata ifikapo Juni 10 na ameagiza kuwepo kwa mikutano ya masuala ya ulinzi na usalama ambayo itakuwa ikijadili ulinzi na usalama na matukio yaliyojitokeza na namna yalivyoshughulikiwa pia ametaka uwepo wa kitabu ambacho kitakuwa kinaonyesha namna wananchi waliofika ofisini na namna kero zao zilivyotatuliwa.
Aidha amewataka viongozi hao kutambua kuwa miradi yote inayofanyika katika maeneo yao inawahusu na wanapaswa kuifahamu vizuri huku upande wa elimu akiwataka viongozi hao kuhakikisha watoto wote wanaostahili kusoma wanapata haki ya kupata elimu ambapo pia ametaka ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari kuanza mapema.
Upande wa migogoro ya wakulima na wafugaji ametaka viongozi hao kuendelea kusimamia utii wa sheria kwa kuhakikisha usalama na amani inadumu katika maeneo yao jambo litakalosaidia wilaya kuwa na utulivu na amani huku akitaka hatua za haraka kuchukuliwa pindi tatizo linapojitokeza ili kutoleta taharuki na hasira katikati ya jamii.
Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila
Kaimu Meneja Mamlaka ya Mapato Kilosa Mussa Haruni
Naye Katibu Tawala Yohana Kasitila ametaka watendaji hao kuhakikisha miongoni mwa ajenda zinazokuwepo katika vikao vyao ni ajenda ya ulinzi na usalama, mapato na matumizi, miradi ya maendeleo na huduma za jamii huku Kaimu Meneja wa mamlaka ya mapato(TRA) Mussa Haruni amewasihi watendaji hao kutoa ushirikiano katika kutoa hamasa kwa wananchi kulipa kodi stahiki, kutoa vitambulisho kwa watu stahiki pamoja na kuwakumbusha wananchi kudai risiti kwani kutodai risiti ni kosa kisheria.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa