Wananchi wametakiwa kutambua jitihada mbalimbali ambazo serikali inazifanya katika kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira mazuri ikiwemo katika kuwaletea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi na kwamba jambo lolote linalofanywa na wananchi kwa ajili ya maendeleo serikali haitosita kuliunga mkono.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh, Hamad Masauni alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mikumi ambapo amesema Serikali imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuendeleza miradi mbalimbali, huku akisema kuwa Serikali ya awamu ya sita imejipanga kwa dhati kuwahakikishia wananchi usalama wao na mali zao kwa kuendelea kujenga vituo vya polisi na nyumba za polisi katika maeneo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiusalama.
Akizungumzia suala la migogoro ya wakulima na wafugaji ambalo pia linahusisha jeshi la polisi katika kuzuia vurugu na migogoro hiyo ametaka kila kiongozi mwenye mamlaka katika eneo lake kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro hiyo huku akitaka polisi kata kuweka juhudi za makusudi katika kutimiza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu,sambamba kutoa elimu ya ulinzi shirikishi kwa wananchi lakini pia kukemea na kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaohusika na kesi mbalimbali za ubakaji ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Aidha amelitaka jeshi la magereza kuwekeza zaidi katika kuendelea kutumia rasilimali walizonazo katika kuisadia Serikali kutimiza adhma yake ya kuhudumia wananchi kwani jeshi hilo lina wataalam wakutosha ambao wana uwezo wa kusababisha mabadiliko chanya kwa jamii na Serikali kiujumla.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumu Mh Dennis Londo ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa fedha nyingi ambazo Jimbo la Mikumi limepokea kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini pia amemuomba waziri huyo kuongeza nguvu katika kuiesema miji ambayo inapaswa kupewa hadhi ya kuwa halmashauri kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa miradi ya kimkakati huku akiomba kufanyika kwa maboresho ya upatikanaji wa kituo kikubwa cha polisi pamoja na vituo vidogo kwa baadhi ya maeneo kwani maeneo mengi ya wilaya hayana vituo vidogo vya polisi,uboreshwaji wa njia za mawasiliano huku akishauri kufanyika kwa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kilosa-Mikumi jambo litakalosaidia wananchi kutotumia umbali mrefu kuelekea maeneo mbalimbali.
Kwa upande wa viongozi wa jeshi la Magereza Mkuu wa gereza mkoa wa Morogoro ACP Dkt. Wilson Rugamba na Mkuu wa gereza Kilosa ASP Dominick Mshana wamesema jeshi la magereza liko tayari kutekeleza na kupokea mabadiliko chanya yanayoendelea ndani ya Serikali na kwamba wanajipanga kuwa na jeshi la kisasa lenye tija kwa ajili ya kuzalisha hususani katika kilimo kwa kutumia rasilimali zilizopo kutokana na ardhi ya kilimo waliyonayo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa