Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye Sekta ya Afya na Elimu benki ya NMB imetoa msaada wa Madawati,Viti, Meza na Vifaa tiba ikiwemo Mashine za kupimia presha,Magodoro, na Mashuka yenye thamani ya Shilingi Milioni 33.1.
Akizungumza Agosti 27,2024 mara baada ya kukabidhiwa Msaada huo katika Kituo cha Afya Kimamba na Shule ya Sekondari Chanzuru Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amesema Banki ya NMB imekuwa ikishirikiana na Jamii wakati wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika wilaya hiyo na kuutaka uongozi na Jamii kwa ujumla kuvitunza vifaa hivyo ili vitumike kwa muda mrefu.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael John Gwimile ameishukuru Bank ya NMB kwa msaada huo na kusema kuwa vifaa hivyo vitakwenda kuboresha sekta ya elimu huku akiwataka wanafunzi hususani kidato cha nne kusoma kwa bidii ili kupata ufaulu mzuri katika Mitihani yao ya mwisho.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Wilfred Sumari amesema Bank ya NMB imekuwa ikijali jamii wakati wa changamoto mbalimbali na kutoa michango mbalimbali pale inapohitajika kufanya hivyo, na kwa upande mwingine ameupongeza Uongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Naye Meneja wa Bank ya NMB kanda ya Kati Bi. Janeth Shango amesema Bank ya NMB inayo Sera ya kurejesha kwa jamii faida inayopatikana ili kuboresha Huduma muhimu kwa wananchi katika sekta mbalimbali kama vile Elimu, ambapo hutoa madawati kwa shule za msingi, viti na meza kwa shule za Sekondari na vifaa vya kuezekea kwa shule zote, na kwa upande wa Sekta ya Afya huchangia Vifaa tiba vinavyohitajika katika eneo husika sambamba na kutoa msaada pindi Maafa yanapojitokeza katika maeneo mbalimbali.
Bi. Janeth ameongeza kuwa Bank ya Nmb imeweza kukabidhi madawati 235 kwa ajili ya shule za Msingi 4 ambazo ni Dakawa Senta 65, Tindiga 60, Malangari 50, Mbigiri 60 pamoja na viti 50 na meza 50 kwa ajili ya shule ya Sekondari Chanzuru sambamba na vifaa tiba Magodoro 60, Mashuka 60 na Mashine za presha 3 vyenye thamani ya shilingi milioni 33. 1.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa