Taasisi ya Utafiti na Kilimo Tanzania (TARI) imeshauriwa kuongeza kasi katika kufanya tafiti zinazokidhi mahitaji ya wakulima ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa Sekta ya Kilimo.
Wito huo umetolewa 23 Februari, 2024 na naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde alipotembelea kituo cha utafiti cha TARI Ilonga kilichopo wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro.
Mhe. Silinde amesema kuna hitaji la upatikanaji wa mbegu bora za kilimo kwa wakulima zenye kuendana mabadiliko ya tabia nchi na kuhimili magonjwa hivyo kuwataka watafiti kuongeza jitihada za kufanya tafiti na kusambaza teknolojia za kilimo.
Kulifikia lengo hilo Mkurugenzi Mkuu TARI Dkt. Thomas Bwana amesema TARI imejipanga kutafiti na kusambaza teknolojia za kilimo zenye kukidhi mahitaji huku wakiendelea kuwekeza katIka kuandaa wataalam na kufanya tafiti zinazotatua changamoto mbalimbali za kilimo.
Dkt. Bwana ameongeza kuwa TARI inamiundo mbinu ya kisasa ambayo inaendelea kuboreshwa ikiwemo maabara na mashamba ya kufanyia tafiti katika maeneo mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa kituo cha TARI Ilonga wilayani humo Dkt. Emmanuel Chilagane ametumia fursa hiyo kuhamasisha wakulima kuendelea kutumia teknolojia zinazogunduliwa na TARI zenye kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Mkinga ameipongeza TARI kwa jitihada zake na kusema kuwa kupitia kituo hicho cha TARI Ilonga kimeongeza uzalishaji wenye tija katika mazao mbalimbali yanayostawi ukanda huo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa