Baraza Maalum la Madiwani limefanyika Juni 11, 2025 katika ukumbi wa FDC Ilonga, Wilayani Kilosa, kwa ajili ya kupitia na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Katika kikao hicho, jumla ya hoja 20 ziliwasilishwa na kujadiliwa; kati ya hizo, hoja 3 zimefutwa rasmi, hoja 7 zimekabidhiwa Halmashauri kwa ajili ya kufanyiwa kazi ili zifutwe, huku hoja zilizobaki zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, ambaye ameendesha kikao hicho na kutoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka kuhakikisha miundombinu ya ukusanyaji mapato inawekwa katika stendi za maroli za Mikumi na Dumila ndani ya wiki mbili.
Mhe. Malima amesisitiza kuwa maeneo hayo yawe vyanzo vya mapato ya halmashauri ambapo pia amemuagiza Afisa Ardhi Wilaya Ndg. Hilal Hamisi Iddi kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji, akieleza kuwa Kilosa itakuwa lango la utalii kuelekea Hifadhi ya Mikumi.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Mussa Ally Mussa amesisitiza kukamilishwa kwa majengo ya halmashauri, ukumbi wa halmashauri, na majengo ya hospitali ya wilaya kwa haraka huku akiwakumbusha madiwani kutumia vishikwambi walivyopewa kwa matumizi ya ofisi ili kuhifadhi nyaraka za serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa na madiwani kwa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pia amewatakia mafanikio mema katika uchaguzi mkuu ujao.
Baraza hilo limeonyesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha uwajibikaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Kilosa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa