Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wabia wa sukari ambao ni NSSF pamoja na Jeshi la Magereza kuhakikisha serikali inafikia malengo ya uzalishaji sukari kwa kiwango kinachotarajiwa kwa kuzalisha tani 485,000 ifikapo 2020 ikiwa ni mahitaji ya sukari ya majumbani kwani kwa sasa serikali inatumia fedha nyingi kuagiza sukari nje ya nchi, hivyo njia pekee kufikia malengo hayo ni kuwa na shamba kubwa la miwa, kiwanda na mashine itakayokamua miwa hiyo ili kufanikisha upatikanaji wa sukari.
Majaliwa amesema kuwa kwa sasa kiwango kinachozalisha ni tani 345,000 hivyo ameitaka menejimenti mpya ya NSSF pamoja na bodi mpya ya Mkulazi kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza ambao ni wabia kutoka na mpango thabiti wa kusimamia mashamba ya Mkulazi 1 na 2 yaanze kazi mara moja kwa kuimarisha mifumo yote ya maji ili kuyakusanya yasaidie wakati wa kiangazi, upatikanaji wa mashine za umwagiliaji wakati wa kiangazi.
Aidha amesema ushiriki wa Magereza ni mzuri na amelitaka jeshi hilo kuleta wataalam wa kilimo watakaosimamia kitaalam na kuwa shamba hilo la Serikali liwe shamba la mfano na kuwa na usimamizi wa kutosha ikiwemo upatikanaji wa mashine za uvunaji na usagaji miwa kiwandani na kwamba wanakilosa wawe na mategemeo ya kujifunza kilimo hicho cha miwa ili walime kwa tija.
Aidha amewataka wakazi wa Kilosa na maeneo ya jirani kutumia fursa ya kilimo hicho cha miwa kujifunza na kulima kitaalam kwani vitendea kazi vipo, usimamizi na ushauri utapatikana kupitia wataalam watakaopatikana katika shamba hilo la miwa na kwamba miwa watakayolima itapeleka kiwandani na kuchakatwa jambo litakaloinua uchumi wa mtu mmoja mmoja huku serikali ikipata mapato.
Sambamba na hayo Waziri Mkuu amewaagiza wakurugenzi wote nchini kuhakikisha maafisa kilimo wote nchini hawakai ofisini badala yake wasambae katika kata na vijiji yalipo mashamba ili kuwasaidia wakulima katika namna bora ya kulima kisasa ili waweze kupata tija kupitia kilimo na ametoa wito kwa watumishi wa umma kulima ili kujiongezea kipato kwani ardhi ya kutosha ipo.
Katika ziara yake Waziri Mkuu ameambata na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu Mh. Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Omary Mgumba.
Akisoma taarifa yake mbele ya Waziri Mkuu Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Mkulazi Hildelitha Msita amesema kuwa baada ya bodi hiyo kuteuliwa aziri mkuu alitoa maagizo kwa bodi hiyo ambapo kwa sehemu kubwa wamyafabyia kazi ikiwemo kumpata meneja wa mradi, ambapo kwa sasa wanaendelea na usaili wa wafanyakazi upande wa manejimenti, wameshapata wataalam wa kilimo, pia msukumo wao upo katika kupata wakandarasi watakaoweka mitambo ya uhakika, na kwamba ukaguzi wa kampuni umeshafanyika na upembuzi yakinifu wa mradi umefanyika na kwamba licha ya kufanyia kazi maagizo hayo ipo changamoto ya miundombinu ya umeme pamoja na uhakika wa mashine za kiwandani hapo sambamba na uhaba wa mvua kwa mwaka huu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa