Viongozi wapya wa serikali za mitaa waliopitikana kupitia uchaguzi ulifanyika uliofanyika Novemba 27 na 28, 2024 wameapishwa rasmi leo tarehe 29 Novemba, 2024.
Viongozi hao, wakiwemo wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wa kundi mchanganyiko wamekula kiapo cha utii na uadilifu katika kata mbalimbali ikiwemo tindiga, Masanze, zombo, Ulaya, Mhenda na kisanga wilayani humo.Hafla hiyo ilifanyika chini ya usimamizi wa Mhe. Hakimu Mkazi Martin Morris Cyprian.
Mhe. Hakimu Martin Cyprian, ambaye alisimamia kiapo hicho, aliwakumbusha viongozi hao kuwa kiapo walichokula si jambo la kawaida bali ni ahadi rasmi inayowalazimu kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwamba kushindwa kutimiza ahadi hizo ni sawa na kukosa kuheshimu dhamana ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Betuely Joseph Ruhega amewakumbusha viongozi hao umuhimu wa kutambua dhamana waliyopewa na wananchi na kuwataka viongozi hao kuonyesha uadilifu, uwajibikaji na kutanguliza maslahi ya jamii katika kila hatua ya uongozi wao.
Aidha Ruhega alisisitiza kuwa viongozi hao ni watumishi wa umma, hivyo wanapaswa kusimamia miradi yote ya maendeleo, kuhakikisha mapato ya vijiji yanakusanywa na kuwekwa benki na viapo hivyo vya utii vikawe tija kwa wananchi.
Baadhi ya watendaji waliokuwepo kwenye hafla hiyo nao walitoa wito kwa viongozi hao kuhakikisha wanachukua hatua zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi waliowachagua.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao ni mwanzo wa safari mpya ya maendeleo katika wilaya ya Kilosa ambapo Halmashauri ya Wilaya hiyo inawataka viongozi hao kushirikiana na wananchi ili kufanikisha malengo ya maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa