Wananchi na Wadau mbalimbali wa maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ,( Nanenane) wamewatakiwa kutekeleza kwa vitendo ujuzi, maarifa na teknolojia mpya walizopata katika kipindi chote cha maonesho hayo ili waweze kuongeza tija na thamani ya mazao yatokanayo na sekta hizo.
Agizo hilo limetolewa Agosti 8, 2025 na Balozi Dkt. Batilda Burian Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika Viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, vilivyoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema,Wananchi wanapaswa kuyatumia kikamilifu maarifa waliyoyapata wakati wa maonesho, hususan yale yanayohusu teknolojia za kisasa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ili waweze kuongeza kipato chao na kukuza uchumi na pato la Taifa kwa ujumla .
Aidha, amewataka viongozi wa Serikali kutoyachukulia maonesho ya Nanenane kama mzaha, kwani kufanya hivyo ni kunapoteza malengo msingi ya maonesho hayo badala yake wayatilie mkazo ili yawe chachu ya katika kutoa elimu ya kisasa kwa wananchi, ikiwemo mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema Kanda ya Mashariki inajipanga kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa ya mfano kwa kutekeleza na kusambaza teknolojia zilizowasilishwa katika maeneo mbalimbali ya kanda hiyo ili ziweze kutumika kwa manufaa ya Halmashauri zao.Aidha, Mhe. Malima amesema katika maonesho hayo kulikuwa na jukwaa la biashara lililojulikana kwa jina la B2B (Business to Business) amesema jukwaa hilo limewakutanisha wataalamu zaidi ya 1,200 wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na taasisi mbalimbali, ambao walipata elimu watakayopeleka maeneo yao kwa lengo la kuongeza thamani katika sekta hizo.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima amewashukuru Wadau waliofanya Maonesho mwaka huu huku akisifu kuwa yamekuwa mazuri na yenye mvuto mkubwa na kwamba takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya Watu laki moja wametembelea Mabanda katika maonesho hayo na kwamba idadi hiyo ni mafanikio ambayo hayajawahi kufikiwa hapo awali.
Maonesho hayo yameongozwa na kaulimbiu isemayo "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 2025" .
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa