Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro Euphrasia Buchuma amewataka Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kusimamia na kuendesha Mafunzo ya Walimu Kazini (MEWAKA) ili kujengeana uwezo na kufanya tathmini za mara kwa mara zikiwemo tathmini za upimaji na maendeleo ya wanafunzi.
Wito huo ameutoa Julai 25, 2024 wakati wa kikao cha Tathmini ya Ufuatiliaji wa Taaluma kilichofanyika katika ukumbi wa Mamboya Kilosa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na wasimamizi wa elimu ngazi za kata na shule.
Amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa walimu huwasaidia walimu kufanya tathimini na kujengeana uwezo katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo kufanya mapitio ya upimaji kabla na baada ya kufanya mitihani.
Aidha Bi. Buchuma amewataka walimu kuboresha mfumo wa lishe shuleni ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu kwa kushirikiana na wazazi au walezi wa kuwapatia chakula wanafunzi na kuzitaka shule zenye maeneo ya kufanya kilimo, zilime ili kuzalisha chakula chao zenyewe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael Gwimile amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kushughulikia baadhi ya hoja zilizobainishwa kwenye tathmini hiyo.
Aidha amewataka walimu kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi yao kwani ni kada inayotegemewa na taifa kuzalisha wataalamu mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa