Wananchi wilayani Kilosa wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti, ili kuweza kubaini ugonjwa huo mapema na kuanza matibabu kwa wakati.
Wito huo umetolewa Oktoba 1, 2025 wakati wa mafunzo maalum kwa viongozi wa kata na viongozi wa dini kupitia mradi wa Beat Breast Cancer unaotetekelezwa na jhpiego kwa kushirikiana na wizara ya Afya kwa kufadhili na Pfizer Foundation yaliyofanyika katika maktaba ya Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Salvatory Kyara, Daktari wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, amesema saratani ya matiti ni ugonjwa hatari unaosababisha vifo vingi, lakini unaweza kutibika endapo utagundulika mapema.
Aidha amesema kuwa saratani hiyo husababishwa na kurithishana vizazi na vizazi, mtindo wa maisha usiofaa, lishe duni, matumizi ya pombe, sigara, kutonyesha maziwa ya mama, kuzaa ukiwa na umri mkubwa n.k
Naye Afisa Muuguzi Joyna Vitus Mlwale, ambaye pia ni Kaimu Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa kata juu ya namna ya kutambua dalili za awali za saratani ya matiti, visababishi vyake, na namna sahihi ya kujipima ili kuongeza uelewa na kuhamasisha jamii katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Saimon Bartazar Swai, Katibu wa Afya Wilaya (akimwakilisha Mganga Mkuu wa Wilaya), ameishukuru taasisi ya Jhpiego kwa kufanikisha mafunzo hayo muhimu, huku akisisitiza kuwa elimu hiyo ifikishwe kwa jamii kupitia watendaji waliopata mafunzo kwa matokeo chanya.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa