Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule Msingi wilayani Kilosa wametakiwa kutekeleza na kusimamia vema majukumu yao na kufanya tathimini ya kina juu ya maendeleo ya kielimu katika shule zao hasa upande wa kitaaluma ili kuleta matokeo chanja kama ilivyokusudiwa.
Hayo yamebainishwa January 26, 2024 katika ukumbi wa Mamboya kata ya Kilosa Mjini na Mkuu wa divisheni ya Elimu Msingi Bi Zakia Fandey katika kikao kazi cha tathimini ya mitihani ya darasa la nne na darasa la saba 2023, ambapo pia ni kikao cha kwanza cha utekelezaji Elimu Msingi.
Ameeleza kuwa endapo Afisa Elimu na wakuu wa shule wakiongeza bidii katika ufatiliaji wa karibu wataweza kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi na walimu na kuzitatua kwa wakati katika shule zao itaondoa adha ya kushuka kitaaluma na kuleta matokeo au ufaulu wa kiwango cha juu.
Sambamba na hayo amezipongeza baadhi ya shule zilizoingia kumi bora kiwilaya katika mitihani ya darasa la saba kwa ufaulu wa asilimia 77.32 ambapo shule hizo ni kama vile Bichop Chitemo, St. peters clavery, Miyonga, Amani, Kantui, King vision, Kikoboga, Mambegwa, Mabwegere na Ruaha B na kuwataka waongeze jitihada zaidi kwa kushika nafasi za juu kimkoa mpaka ngazi ya kitaifa pia ameshauri kwa baadhi ya shule ambazo hazikuingia kumi bora wajifunze kupitia shule hizo ambazo ni mfano wa kuigwa.
Pia amesisitiza walimu kuendelea na zoezi la uandikishaji kwa elimu ya awali katika kata zote 40 na kufikia lengo lilokusudiwa, hivyo ameshauri walimu kuendelea kuhamasisha wazazi kuleta wanafunzi shuleni.
Naye Afisa Elimu watu wazima Richard Mpumilwa amewakumbusha Wakuu shule kutunza mazingira ya shule kwa kupanda miti na maua, kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na rafiki kwa mwanafunzi kusoma ili kuzuia magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Pia ameongeza kuwa ili kupunguza adha ya uchache wa madawati, Afisa Elimu kata wajitahidi kufatilia na kuomba vibali kwa uongozi wa kata kupata vibali vya uvunaji wa miti ili kupata mbao za kutengenezea madawati na kupunguza changamoto za uchache wa madawati katika shule hizo.
Kwa upande wake Katibu Msaidisi wa Tume ya Utumishi ya Walimu Daud Mchillu Amewataka waalimu kuwa waadilifu, kuwa na mahusiano mazuri katika vituo vyao vya kazi pia kufanya kazi kwa ushirikiano bila kutumia nguvu ya Madaraka vibaya. Pia amewaasa walimu kupunguza kuchukua mikopo katika taasisi mbalimbali au kampuni binafsi zinazokopesha na kusababisha madeni kandamizi na kupelekea udhaifu katika utendaji kazi.
Kikao hicho Kwa pamoja kimeazimia Kuendelea kuwajengea uwezo Walimu kupitia Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini ngazi ya shule, kata na Klasta ili kumudu masomo wanayofundisha pia Kuendelea kubaini wanafunzi watoro na kuwasilisha taarifa kwa Watendaji wa Kata kwa ajili ya kuchukua hatua kwa Wazazi wanaoshindwa kusimamia watoto wao kwenda shule. Pia kuwaelimisha wazazi au walezi wanapotaka kuhama kuzingatia taratibu za uhamisho wa Mwanafunzi.
Aidha Jitihada zaidi zimetakiwa zifanyike ili kuboresha ufaulu wa masomo ya Hisabati, Kiingereza, na Sayansi na Teknolojia.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa