Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Kilosa kwa kuipatia miradi mbalimbali ikiwemo miradi iliyotembelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh.Innocent Bashungwa ambapo alitembelea ujenzi wa shule ya Sekondari iliyopo kata ya Berega almaarufu shule ya Sekondari Kabudi ambayo imepelekewa shilingi bilioni moja, ujenzi wa daraja la Berega lenye urefu wa mita 140 litakalogharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.9 pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nhembo kilichopo katika kata ya Mabula kilichopelekewa shilingi milioni 700.
Baadhi ya majengo ya shule ya sekondari(Kabudi sekondari) katika kata ya Berega ambayo ujenzi unaendelea.
Akiwa katika shule ya Sekondari Kabudi Julai 23, 2022, Mh. Bashungwa amemuagiza Mkuu wa MKoa wa Morogoro Martine Shigela kusimamia kamati mbili zilizoundwa kuangalia matumizi ya fedha shilingi bilioni moja zilizoletwa na Serikali katika shule hiyo kwa ajili ya kidato cha tano na cha sita kama matumizi yake yamefuata taratibu na miongozo iliyopo na kuiwasilisha taarifa ya kamati hizo ofisini kwake, huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuanza maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyoambao wataanza masomo yao mwezi Septemba 2022 kwa kuhakikisha vyumba vya madarasa vinakamika na kuwa tayari kwa matumizi.
Baadhi ya majengo ya ujenzi unaoendelea kituo cha Afya Nhembo kata ya Mabula
Kwa upande wa ujenzi wa kituo cha afya Nhembo katika kata ya Mabula Bashungwa amepongeza ujenzi wa kituo hicho ambacho kitaondoa kero ya wananchi kutembea umbali mrefu kwenda kufata huduma za afya ambapo kwa sasa wananchi hutembea umbali mrefu jambo ambalo limekuwa adha kwa wananchi kwa muda mrefu huku akiwapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kushiriki kikamirifu katika ujenzi wa kituo hicho.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa daraja la Berega ambalo limekuwa changamoto kubwa ya ukosefu wa mawasilianokwa wananchi wa kata ya Belega kwa muda mrefu na kusababisha vifo vya wananchi Bashungwa amemtaka mkandarasi anayejenga daraja hilo Nyanza Road Works Ltd kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Juni 2023 kama mkataba unavyoonesha ambapo pia amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA Mkoa wa Morogoro kusimamia ukamilishaji wa mradi huo kwa muda uliopangwa.
Sambamba na hayo amemuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro kufanya afiti matengenezo ya maeneo yasiyopitika kiurahisi barabara hiyo ambayo inaunganisha Wilaya ya Kilindi Mkoa Tanga ili yaboreshwe ili daraja hilo liweze kuwa na tija kwa Wilaya za Kilosa na Gairo za Mkoa wa Morogoro na Kilindi na Handeni kwa Mkoa wa Tanga.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akifafanua kuhusu hatua zilizochukuliwa juu ya ujenzi wa shule ya sekondari Kabudi amesema zimeundwa timu mbili zitakazohusika na ukaguzi ili kujiridhisha na manunuzi ya vitendea kazi ikiwa yalifuata kanuni na taratibu, huku kamati nyingine ikijikita upande wa utalaam wa uhandisi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha za miradi hiyo jimboni kwake hususan ujenzi wa daraja la Berega ambalo ni muhimu sana kwa mustakabali wa maisha ya wananchi wa kata ya Berega na kata nyinginezo kwani daraja hilo limekuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu.
.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa