Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) katika Wilaya ya Kilosa wameushukuru mradi huo kwa kuboresha maisha yao kwa kipindi cha miaka kumi, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013. Wameeleza kuwa ruzuku na miradi ya kuwezeshwa kiuchumi vimewasaidia kujikwamua kutoka katika hali ngumu ya maisha.
Wakizungumza katika Kijiji cha Rudewa Agosti 19,2025 wanufaika wamesema kuwa pamoja na mradi huo kukamilika mwezi Septemba mwaka huu, bado wana mahitaji ya msingi yanayohitaji msaada wa Serikali. Wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuendeleza mpango huo au kuanzisha awamu nyingine ili kuwasaidia zaidi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Rudewa, Masudi Msabaha, amesema mradi wa TASAF umeleta mageuzi makubwa kwa wananchi wake, ambapo baadhi yao wameweza kujenga nyumba bora, kulipia ada za watoto na kuanzisha shughuli ndogondogo za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwezeshaji wa TASAF ngazi ya wilaya, Bi. Mwanaidi Rajabu, amesema jumla ya kaya 10,316 zilisajiliwa katika vijiji 138 vilivyopo Kilosa, na zaidi ya wanufaika 35,000 wamepata ruzuku pamoja na kupewa fursa ya kujiunga na vikundi vya kuweka akiba na kujiendeleza kiuchumi.
Naye Mratibu wa TASAF wilayani humo, Dedan Maube, amesema malipo ya sasa ni ya mwisho kwa awamu hii ya mpango, na walengwa pia wamepatiwa bonasi kama sehemu ya kuhitimisha utekelezaji huku akiwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa uangalifu na kuzielekeza kwenye shughuli zenye tija kiuchumi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa