Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka amekabidhi hundi ya mfano ya Shilingi milioni 541.3 kwa vikundi 38 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Hafla hiyo ya utoaji mikopo imefanyika Agosti 27, 2025 katika viwanja vya Halmashauri hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wanufaika wa mikopo hiyo.
Akizungumza baada ya kukabidhi hundi hiyo, Mhe. Shaka ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyokuwa na riba.
Aidha, amewataka wanufaika kuhakikisha fedha hizo zinatumika katika shughuli za kiuchumi na sio kwa matumizi yasiyo na tija, huku akisisitiza ulazima wa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili wengine waweze kunufaika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Bi Beatrice C. Mwinuka, amewahimiza wanavikundi kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kuhakikisha wanarejesha marejesho kwa wakati na amesema bado kuna vikundi vingi vinavyosubiri kupata mikopo, hivyo ni wajibu wa kila mnufaika kuhakikisha fedha hizo zinarudi kwa wakati ili mzunguko uendelee.
Naye Mratibu wa Mikopo ya asilimia 10 Kilosa, Ndg. William Mlay, amesema vikundi vyote vilivyopata mikopo vilikidhi vigezo na vimepatiwa elimu ya ujasiriamali na namna bora ya kutumia na kurejesha mikopo hiyo na zoezi hilo linaendelea kwa awamu ili kuhakikisha makundi mengi zaidi yanahusishwa.
Pia Afisa TAKUKURU Wilaya ya Kilosa, Ndg. Elias Masila, ametoa onyo kwa wanufaika watakaojaribu kutumia fedha hizo kwa matumizi yasiyofaa au kughushi nyaraka, akisema taasisi hiyo itasimamia kwa ukaribu matumizi ya fedha hizo ili kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa.
Kwa niaba ya vikundi vilivyopokea mikopo hiyo , Bi Yusta Bernad kutoka kikundi cha Wanawake na Maendeleo Ilonga kata ya Chanzuru, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mitaji itakayowawezesha kukuza biashara na kuinua kipato na kueleza kuwa fursa hiyo ni kichocheo muhimu kwa maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa