Katika kikao cha utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa robo ya nne (Aprili–Juni 2025) kilichofanyika Agosti 20, 2025 Wilayani Kilosa, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa kata zote kuongeza juhudi katika kuhamasisha wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni.
Kikao hicho kimewakutanisha watendaji wa kata, wataalamu wa lishe, na viongozi mbalimbali kujadili maendeleo ya lishe mashuleni.
Taarifa iliyotolewa imeonesha kuwa baadhi ya kata hazijafanya vizuri katika utoaji wa chakula mashuleni kutokana na changamoto ya viongozi kushindwa kuwashawishi wananchi kuona umuhimu wa kuchangia chakula kwa watoto wao. Mkuu wa Wilaya huyo amesema suala la lishe bora shuleni ni la lazima kwa maendeleo ya elimu na afya za watoto na amewataka wakuu wa shule kuhakikisha chakula kinatolewa kwa usalama na kuwa na virutubisho stahiki.
Afisa Lishe Wilaya ya Kilosa, Elisha Kingu, akitoa taarifa ya viashiria vya lishe, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaopata chakula shuleni kutoka asilimia 64.03 katika robo ya tatu hadi asilimia 84.87 kwa robo ya nne, jambo linaloonesha mafanikio ya juhudi za uhamasishaji. Hata hivyo, ameongeza kuwa bado kunahitajika juhudi zaidi kuhakikisha shule zote zinatoa chakula.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bi. Beatrice C. Mwinuka ametoa rai kwa watendaji wa kuwajibika katika maeneo yaowananyoyasimamia kwa kuetekeleza vyema suala la lishe mashuleni kwa asilimia mia moja (100).
“Viongozi ongezeni jitihada na uwajibikaji kusimamia vyema suala la lishe mashuleni “ Alisisitiza Bi. Beatrice
Aidha, Mtendaji wa Kata ya Masanze kwa niaba ya watendaji kata amesema wamepokea maelekezo hayo na wako tayari kuyaleta kwenye vikao vya vijiji ili wazazi waelimishwe juu ya umuhimu wa kuchangia chakula. Wazazi wengi, amesema, huona ni mzigo lakini ukweli ni kwamba ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa maendeleo ya watoto wao.
Afisa Kilimo Bi Zena Omary amewataka watendaji kushirikiana na maafisa kilimo katika kuanzisha bustani shuleni kwa shule zisizo na uwezo wa kifedha. Amesema njia hiyo itasaidia kupatikana kwa mboga na mazao ya chakula shuleni kwa gharama nafuu, huku ikiwajengea wanafunzi uelewa wa kilimo cha bustani.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa