Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina amezitaka Halmashauri zote nchini kuboresha na kukarabati Machinjio,Milaro, Malambo, Majosho pamoja na minada ya Mifugo kwa kuweka huduma muhimu kama vile vyoo, umeme na sehemu za kuuzia vyakula ili kufanya minada ya mifugo kuwa ya kisasa na yenye tija.
“Tumetoa miezi mitano tu kwa Halmashauri zote nchini kukarabati miundombinu ya Majosho, Malambo,Machinjio pamoja na Minada yote ikarabatiwe iwe bora na yenye huduma zote muhimu na Halmashauri itakayoshindwa kufanya hivyo serikali itasitisha ukusanyaji wa mapato unaofanywa na Halmashauri husika na kuikabidhi kwa serikali kuu.” Alisema Mpina.
Katika hatua nyingine Mpina alitoa siku saba kwa Makatibu wakuu wa Wizara za Mifugo na Uvuvi na Kilimo kueleza ni kwa nini mbegu za mazao zinauzwa kwa bei ghali ambayo inafikia shilingi 6,000/= kwa kilo na uhamilishaji wa mifugo kuwa na bei kubwa ambapo amesema ng’ombe mmoja anahamilishwa kwa zaidi ya shilingi 22,000/=
Siku chache za nyuma katika kipindi cha maonesho ya Nane Nane Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe , amesema kuna maendeleo makubwa ya ukusanyaji wa mapato ya Nanenane Kanda ya Mashariki ambapo Sekretarieti za Mikoa huendesha na kusimamia maonesho hayo ambapo kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2017 takribani shilingi Mil. 200 zilikusanywa wakati mwaka 2016 ambapo maonesho hayo yalikuwa yanaendeshwa na TASO zilikusanywa shilingi Mil.70 tu.
Aidha katibu wa kamati ya maandalizi ya NaneNane kanda ya Mashariki Bw. Ernest Mkongo amesema changamoto zote zilizojitokeza mwaka huu zitafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuhimiza wadau kujenga mabanda ya kudumu pamoja na kuziba sehemu za wazi kuzunguka uwanja wa maonesho ili kuziba mianya ya mapato inayopotea kutokana na watu kuingia bila kutoa kiingilio pamoja na kushirikiana na uongozi wa Mkoa na taasisi zake katika kufanikisha uboreshaji bwawa la Mindu ili kutatua changamoto ya maji katika uwanja wa maonesho wa NaneNane.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa