Rai imetolewa kwa Uongozi wa CAMFED kuongeza juhudi katika kuhakikisha wanaendelea kuifikia jamii hususani kwa mikoa ambayo bado haijafikiwa na huduma zinazotolewa na CAMFED ambapo wametakiwa kuhakikisha msichana anapata elimu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika utoaji wa elimu kwa watoto wa kike.
Rai hiyo imetolewa Agosti 30 mwaka huu na Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo toka Wizara ya Kilimo Mashaka Mdangi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kilimo na ujasiliamali kwa washiriki waliofadhiliwa na CAMFED toka mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga na Iringa ambapo mafunzo hayo ya siku kumi yanafanyika katika chuo cha Kilimo Mati Ilonga.
Mdangi amewataka washiriki hao kutoa elimu kwa jamii kile watakachojifunza ili kusaidia wengine kutumia taaluma waliyopata kwa lengo la kupata tija jambo litakalosaidia wao na jamii kunufaika lakini pia jamii watayoihudumia kupata kilicho bora.
Akizungumzia shirika la CAMFED Meneja Mradi Nelly Fute amesema lengo la uwepo wa shirika hilo ni kuhakikisha wanamwezesha mtoto wa kike kupata elimu kwa kumfadhili masomo yake ya sekondari dhidi ya changamoto mbalimbali zinazomkabili katika maeneo mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa sare za shule, usafiri, madaftari lakini pia kuhakikisha wanafunzi wote wanaofadhiliwa na CAMFED wanajifunza stadi za maisha katika shule za sekondari kupitia program ya Dunia Yangu Bora, huku wanufaika CAMFED wakisaidiwa kuanzisha na kukuza biashara zao ili wasiwe tegemezi na kwamba wanaishukuru Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikishirikiana nao ikiwemo fursa ya kupata mafunzo katika chuo cha kilimo na kwamba wanaamini mafunzo hao yatawasaidia kujikwamua na kufanya shughuli zao kitaalam zaidi.
Naye Mkufunzi Mkuu wa mafunzo hayo toka Mati Ilonga Mariam Maranda amesema kupitia mafunzo hayo watahakikisha kila mshiriki anakuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya mazao anayojishughulisha ikiwemo kuongeza ubora wa mazao, kuongeza mavuno, namna ya kufanya biashara kwa tija pamoja na utafutaji wa masoko ambapo katika mafunzo hayo watatoa elimu katika makundi ya mazao ya mizizi na nafaka, mazao ya mboga mboga na mazao ya viungo.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Mati Ilonga Felix Mrisho amesema wamejipanga kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za utatuzi wa tatizo la ajira kwani kupitia mafunzo hayo yatasaidia kwa asilimia kubwa kupunguza tatizo la ajira nchini huku mdau wa maendeleo Dkt. Matokeo Kenendy amewataka washiriki hao kuitumia fursa hiyo vizuri kwa kujifunza na kufanyia kazi yale watakayojifunza ili kujiletea maendeleo binafsi na Taifa kwa jumla.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa