Katika kuadhimisha miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Mwenyekiti wa CCM Wilaya Mh Ameir Mbarak chama hicho kimetoa mabati 200 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kitongoji cha Kikonga katika kata ya Kisanga ili kuwasaidia wananchi waishio katika kitongoji hicho ambao hutembea umbali mrefu ili kupata huduma za kiafya.
Akizungumzia maadhimisho hayo Katibu wa CCM Wilaya Comrade Shaban Mdoe amesema chama hicho kimeona vema kutoa mabati hayo ikiwa ni kutia chachu ujenzi huo utakaogharimu shilingi milioni 68 ambao tayari umeshaanza ambapo amesema wananchi wanapaswa kutiwa moyo kwa kile ambacho wameanza huku akitaka uongozi wa kijiji kutazama ujenzi huo kwa jicho la tatu kwa kuunga mkono juhudi hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Alhaji Majid Mwanga amesema kwa dhima aliyokabidhiwa na Mheshimiwa Rais atashirikiana na kitongoji hicho kwa kuhakikisha unakamilika ili kuwasaidi a wananchi hao wanaokumbana na adha kubwa ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 13 ili kufata huduma za kiafya huku akiiagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha katika zahanati hiyo panajengwa nyumba ya daktari.
Naye diwani wa kata hiyo Mh Hassan Kambenga amesema ujenzi huo unaendelea huku zikifanyika juhudi mbalimbali za kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa kushirikisha Halmashauri katika bajeti zake ambapo pia amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuunga mkono shughuli za maendeleo zinazoendelea katika kata hiyo.
Mganga Mkuu Wilaya Dkt. George Kasibante amesema kwa jitihada kubwa zilizoonyeshwa na wananchi hao zahanati hiyo itasajiliwa kwa mujibu wa taratibu na maandilizi yote kufanyika ya upatikanaji wa vifaa na wataalam kwa ajili ya kutoa huduma za afya na kwamba kwa kadri ujenzi huo unavyoendelea Halmashauri itaendelea kuunga mkono ujenzi huo kwa kushirikisha Serikali Kuu.
Bi Tasiana Mauma na Daniel Bihagara kwa niaba ya wananchi wenzao wamesema kutokuwepo kwa huduma za afya katika kitongoji hicho imekuwa ikipelekea wajawazito kujifungulia njiani lakini pia kutumia gharama kubwa kwenda kufata huduma za afya ambapo wamesema kupitia zahanati hiyo wanaamini itawasaidia kwa matibabu na huduma za uzazi huku wakiiomba Serikali kuwasaidia ili kukamilisha ujenzi huo.
Aidha katika kuunga mkono juhudi za ujenzi huo ambao unaendelea wadau mbalimbali wamejitokeza na kuahidi michango mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu mstaafu wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. George Mlingwa ambaye ametoa mifuko 50 ya saruji, Kudra Ally mzalishaji wa mazao ya misitu ametoa mifuko 9 ya saruji na kuahidi kuchana mbao zote zitakazohitajika kwa ajili ya fremu za jengo zima huku kijiji cha Kisanga kikichangia shilingi milioni moja na Bw. Omari akiahidi kuchimba kisima cha maji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa