Usimamizi mbaya wa wazazi na walezi, wanafunzi kuchelewa kurudi kutoka kwenye mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka pamoja na mwitikio mdogo wa elimu zimetajwa kuwa ni changamoto zinazosababisha baadhi ya wanafunzi katika tarafa ya Mikumi kuchelewa kuripoti shuleni.
Hayo yamebainishwa Januari 8, 2024 na baadhi ya wakuu wa shule za sekondari na msingi mbele ya kamati ya ukaguzi ilipotembelea shule hizo ili kujionea hali ya uandikishaji na upokeaji wa wanafunzi wapya, mahudhurio ya walimu, hali ya miundombinu pamoja na usafi wa mazingira.
“Baadhi ya wanafunzi wanaishi na bibi zao na wengine wanaishi na ndugu zao hivyo ni ngumu kwa ndugu kuifanya shule kuwa kipaumbele, kuna wakati wanafunzi wanakuja wenyewe bila mtu yeyote wa kuwaleta, ukimuuliza anakwambia kuwa yeye anaishi na bibi yake na amekataa kumleta shuleni” amesema Mkuu wa Shule ya Sekondari Mikumi.
Akiongoza kamati hiyo maalumu ya ukaguzi, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka Ngumu na Usafi wa Mazingira Antony Mbisse amesema kuwa kuna haja ya kamati ya shule kwa kushirikiana na viongozi wa dini pamoja na wa serikali za mitaa kuwatangazia wananchi wenye watoto wanaotakiwa kwenda shule wawapeleke shule ili wapate haki yao ya msingi kwani mpaka sasa hali ya uandikishaji hairidhishi.
Katika hatua nyingine amewataka walimu wakuu pamoja na wakuu wa shule za sekondari kuwapokea watoto hata wale ambao hawajakamilisha mahitaji kama vile sare za shule pamoja na vifaa vya kufanyia usafi kwa wale wanaoanza kidato cha kwanza.
Ameongeza kuwa kuna haja ya walimu wanaohusika na masuala ya ushauri nasaha kujiwekea utaratibu wa kukaa na wanafunzi wanaojiunga na shule hizo ili kubainisha changamoto za kifamilia na kijamii zinazosababisha mkwamo wa elimu kwa wanafunzi hao na kuzipatia ufumbuzi
Kamati hiyo imetembelea shule ya msingi, Mikumi, Ruaha A, Ruaha B pamoja na sekondari za Mikumi na Kidodi ambapo kwa shule ya Sekondari Mikumi wameripoti wanafunzi 71 kati 556 waliopangiwa kujiunga na shule hiyo ikiwa ni asilimia 13 pekee, kwa upande wa shule ya Sekondari ya Kidodi wameripoti wanafunzi 96 kati ya 547 waliopangiwa shule hiyo.
Kwa shule ya Msingi Ruaha A walikadiria (maoteo) kupokea wanafunzi mia moja kwa darasa la awali ambapo wameandikishwa wanafunzi 32 pekee na kwa darasa la kwanza wameandikishwa wanafunzi 49 kati wanafunzi mia moja waliokadiriwa kuandikishwa, Shule ya Msingi Ruaha B wameandikishwa wanafunzi 190 kati wanafunzi 200 waliokadiriwa kuandikishwa kwa darasa la awali na darasa la kwanza.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa