Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye ulemavu Mh. Jenista Mhagama Julai 31 mwaka huu ameigiza kampuni ya China Estate kuhakikisha inaweka mazingira bora ya kiafya katika nyumba za zamani za wafanyakazi wa kiwanda hicho hususani suala la vyoo ambavyo kwa sasa vimejaa na kusababisha wafanyakazi hao kuwa hatarini kiafya.
Jenista ametoa agizo hilo alipotembelea kiwandani hapo ambapo amesema kuwa uongozi wa kampuni hiyo unapaswa kuhakikisha kabla ya tarehe 20/08/2019 vyoo hivyo viwe safi na salama kwa matumizi ya wafanyakazi wanaoishi katika nyumba hizo lakini pia ameagiza uwepo wa vitendea kazi na vifaa kinga kwa wafanyakazi ikiwemo vizuia vumbi, gloves, mabuti na visanduku vya huduma ya kwanza ambapo tarehe 20/08/2019 ukaguzi utafanyika kuhakiki utekelezaji wa maagizo hayo.
Pamoja na maagizo hayo Mhagama ameupongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa kujenga nyumba nyingine mpya kwa ajili ya wafanyakazi sambamba na kuwaruhusu wafanyakazi wa kiwanda hicho kufanya shughuli zao za kilimo katika maeneo ya kiwanda ili kujiongezea kipato pamoja na kuwaruhusu uwepo wa wakulima wa nje wa zao la mkonge.
Aidha ametoa rai kwa uongozi kuanzisha viwanda vingine kwa ajili ya bidhaa mbalimbali ili kwenda sambamba na juhudi za Mheshimiwa Rais Jonh Joseph Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda kwani eneo la kiwanda hicho ni kubwa hivyo linakidhi ongezeko la viwanda vingine.
Pamoja na hayo amewahamasisha wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa na mshamba yao ya ziada ili kujiongezea kipato badala ya kutegemea mshahara toka kwa mwajiri wakati fursa ya kutumia maeneo katika kiwanda hicho ipo lakini pia muda wa kufanya shughuli zao upo huku akiwasisitiza kujiunga katika vyama vya ushirika.
Licha ya hayo ametoa wito kwa wawekezaji wote nchini kuhakikisha wanafuata sheria kama inavyostahiki huku akisisitiza wafanyakazi wote nchini kutambua haki zao lakini pia kutimiza wajibu wao kwa kadri inavyostahiki.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa