Chama Cha Walimu wilayani Kilosa kimepongezwa kwa juhudi mbalimbali ambazo imekuwa ikifanya katika kujiletea maendeleo ikiwemo tukio la kihistoria la ununuzi wa chombo cha usafiri wa basi dogo ikiwa ni wilaya ya kwanza kwa mkoa wa Morogoro.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 15, 2024 wakati wa uzinduzi wa basi pamoja na sera ya matumizi ya basi hilo uliofanywa na Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Ndg. Alto Mbikiye kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, ambapo amepongeza chama hicho kwa hatua hiyo ambayo ni mfano wa kuigwa na wilaya nyingine zenye nia ya kujiletea maendeleo.
Akionyesha kufurahishwa kwake na tukio hilo Mbikiye amesema kuwa uwepo wa basi hilo utakuwa chachu ya maendeleo kwa chama hicho, huku akitaka sera ya matumizi ya usafiri huo kusimamiwa vizuri kwa kuepuka upendeleo hususani katika matumizi na kwamba sera ikiheshimiwa na kila mmoja itaepusha migogoro na badala yake itawajenga pamoja kwa umoja, ushirikiano, upendo, mshikamano na amani ndani ya chama.
Akizungumzia suala la malimbikizo ya madai mbalimbali ya walimu Mbikiye amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na kadri fedha inapopatikana inaendelea kupunguza madeni mbalimbali yakiwemo madeni ya fedha za wastaafu na likizo hivyo walimu wote na watumishi wenye madai waendelee kuwa na subra madai yote yaliyohakikiwa yatafanyiwa kazi.
Richard Shagungu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Kilosa amewapongeza wanachama wenzake kwa kufikia makubaliano ya ununuzi wa basi hilo ambayo yamefuata taratibu zote za vikao vya ridhaa na manunuzi huku akisema kuwa anaamini kupitia chombo hicho kitazidi kuwaweka pamoja kama chama na kwamba wanatarajia kuunda kamati maalumu itakayosimamia vema matumizi ya usafiri huo.
Aidha licha ya kuipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ombi kwa Serikali kulitazama kwa upya suala la kikokotoo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa wastaafu hivyo ni vema ukawekwa utaratibu wa kuhakikisha watumishi wa umma pindi wanapostaafu wapatiwe mafao yao yote ya kustaafu ili kuwaweka katika mazingira mazuri kimaisha, huku akipongeza uongozi wa Halmashauri kwa kufanyia kazi kilio chao cha muda mrefu kwa kutenga fedha za matibabu.
Naye Katibu wa CWT Kilosa Andrew Ngazu amewashukuru wanachama wote wa CWT kwa ushirikiano walioutoa katika kusimamia azimio la ununuzi wa chombo hicho ambalo walijiwekea na kulitimiza ndani ya mwaka mmoja jambo ambalo kwao limekuwa ni fahari kubwa ambapo amebainisha kuwa wanachama waliliridhia kutotumia 15% ya mapato yao ya uendeshaji wa shughuli zao kwa lengo la kufanikisha azimio hilo ambapo matumizi ya basi hilo yatazingatia sera inavyosema na kwamba sera hiyo itaendelea kuboreshwa kwa maslahi ya chama hicho ili kujijenga zaidi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa