Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro wamekabidhi mipira 240 katika shule za msingi sita (6) kwa lengo la kuinua na kukuza vipaji kwa wanafunzi mashuleni kuanzia ngazi ya chini ili kuboresha Tasnia ya mchezo wa mpira wa miguu kwa ngazi ya kimataifa.
Hayo yameelezwa leo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Mkinga wakati wa hafla ya kukabidhi mipira hiyo kwa walimu iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa.
Bi. Salome amesema kuwa Serikali imeona vema kukuza vipaji vya michezo kuanzia mashuleni ambapo muwajibikaji wa kukuza vipaji hivyo na kuviendeleza atakuwa mwalimu wa michezo ambapo hatua hii italeta tija katika kukuza vipaji vya watoto wakiwa bado wadogo.
Bi. Salome ametoa Rai kwa walimu na viongozi wa michezo katika ngazi ya wilaya kushirikiana kwa pamoja katika kufanikisha juhudi za serikali na kusema kuwa suala la michezo ni ajira pia ni sehemu ya kujipatia kipato, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanasimamia vyema kukuza vipaji vya wanafunzi ili kuleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) Bw. Pascal Kihanga amesema kuwa serikali kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wameweza kutoa mipira hiyo mashuleni lengo ni kukuza vipaji vya watoto kuanzia ngazi ya chini wakiwa na umri mdogo kuanzia miaka saba badala ya kuwafundisha vijana wenye umri mkubwa ambapo baada ya kufundishwa na kujua kucheza mpira tayari umri wao wa kucheza unakuwa umeisha.
Kihanga amewata walimu kuwa wasimamizi wazuri na kuleta matokeo chanya na watoto watakaofanya vizuri baada ya ufuatiliaji watachukuliwa na kupelekwa kwenye vituo maalum vya mafunzo ambavyo vipo Tanga na Kigamboni.
Sambamba na hayo ameongeza kuwa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kitatoa mafunzo kwa walimu ili kuwajengea uwezo wa kufundisha mpira wa miguu watoto wadogo .
Kwa upande wake Afisa Utamaduni Bi. Paula Katololo amesema michezo hiyo itachezwa kwa kushirikisha jinsia zote mbili wa kike na kiume ambapo mipira hiyo 40 iliyotolewa kwa shule moja itatumika kwa usawa mipira 20 kwa wanafunzi wa kike na 20 kwa wanafunzi wa kiume.
Katika hatua hiyo ya awali shule zilizoanza kupewa mipira hiyo ni pamoja na shule ya msingi Mazinyungu, Ruhembe, Mbamba, Ifunde, Matongole na Ng'ole.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa