Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam I. Mgoyi ametoa agizo kwa wananchi wote wa Tarafa ya Kilosa Mjini kuhakikisha visima vifupi vyote vilivyopo katika makazi ya yao vinafukiwa ndani ya siku kumi na nne kuanzia tarehe 14/08/2018 baada ya kubainika visima hivyo kuwa na kutu ambayo ina madhara kwa wananchi hao ikiwemo kupatwa na kansa ambapo amesema serikali ya awamu ya tano haiko tayari kuona wananchi wakiangamia huku viongozi wakiangalia.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya kwenye mkutano wa hadhara katika Tarafa ya Kilosa Mjini na kusema wamiliki wote wa visima hivyo wanapaswa kuvifukia ndani ya siku kumi na nne na kwamba atakayekaidi agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwani mamlaka ya maji ipo tayari kuwasaidia wananchi namna ya kupata maji na watawaunganishia bure baada ya kukamilisha maelekezo.
’’Lakini pia niseme na nyinyi wazazi ambao watoto wenu wa kike wakibebeshwa mimba mna mtindo wa kuwaficha wanaohusika na mimba hizo kitendo ambacho sio kizuri kwani elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto hasa katika awamu hii ya tano ambapo elimu inatolewa bure, hivyo mzazi atakayebainika kushirikiana na mtuhumiwa wa mimba hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake kwani tendo la kumficha mhusika ni dhahiri linaonyesha kushiriki kupoteza ndoto za mtoto wa kike kupitia elimu ambayo angepaswa kuipata’’. Mgoyi ameongeza.
Sambamba na hayo amewatahadharisha wazazi na wananchi wanaolalamikia suala la upendeleo wa ajira katika kampuni ya Yapi Merkez ambapo amesema hakutakuwa na upendeleo wa aina yoyote kwani watakaofaidika na ajira toka kampuni hiyo ni wale wenye sifa na vigezo stahiki ambao watakuwa wamefanya vema katika usaili wa nafasi mbalimbali zilizotangazwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa