Watendaji wa kata na vijiji wametakiwa kuridhika na kipato wanachokipata kutokana na majukumu yao badala kujihusisha na ukusanyaji wa kipato kisicho halali kupitia makusanyo ya fedha za Serikali kwani Serikali imewaamini na kuwaweka ili waweze kuwahudumia wananchi katika maeneo yao lakini pia kufanya kazi kwa kuheshimiana na kuzingatia nidhamu ya kiutendaji kazi.
Wito huo umetolewa Februari 09/02/2022 na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaj Majid Mwanga wakati wa kikao kazi cha Maafisa tarafa, Watendaji wa kata na Vijiji ambapo amewataka kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma ambao Serikali imewaamini hivyo wanapaswa kufuata sheria, taratibu na kanuni kadri zinavyowaelekeza katika utendaji wao wa kuwahudumia wananchi.
Mwanga amesema wapo baadhi ya watendaji wanaofanya kazi bila kuzingatia taratibu za kazi ikiwemo kukiuka usimamizi wa mapato kama inavyostahiki huku akitoa onyo kwa watendaji ambao wamekuwa wakitumia vibaya madaraka yao badala ya kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia taaluma yao vizuri.
Aidha ametaka kila mtendaji kuweka malengo ya ukusanyaji mapato kwa kila katika eneo lake kwa kuzingatia vyanzo vyote vya mapato vilivyopo katika maeneo yao huku akisisitiza kufanyika kwa zoezi la usafi kila mwisho wa mwezi zoezi ambalo linapaswa kufanyika na watu wote ambapo upande wa mapato amewataka kutambua kuwa moja ya vipimo vinavyotazamwa katika utendaji wao ni ukusanyaji wa mapato ambao kwa sasa umekuwa dhaifu jambo linalopelekea Halmashauri kukusanya kiwango kidogo ilihali mapato yapo ya kutosha ila usimamizi umelegalega.
Pamoja na hayo amesisitiza watendaji hao kutambua kuwa mashine za kukusanyia mapato(POS) ni mali isiyohamishika na kwamba fedha yoyote inayokusanywa kutokana na vyanzo mbalimbali ipelekwe benki mara moja huku akiagiza vizuizi vyote viimarishwe sambamba na kuweka usimamizi mzuri wa magulio yote lakini pia ametaka watendaji hao kuendelea kusisitiza wananchi kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi ifikapo mwezi Agosti 2022 sambamba na kuhamasisha wananchi waweze kupata chanjo ya Uviko-19.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila amewataka watendaji hao kubadilika katika utendaji wa kazi zao hususani katika suala la ukusanyaji mapato kwa kujiepusha namna yoyote ovu na kuepuka rushwa kwani Serikali iko macho hivyo ni vema wakazingatia zaidi sheria, taratibu na kanuni za kazi lakini pia amewakumbusha kuzingatia uandishi wa barua za kiofisi kwa kufuata ngazi za kimadaraka na kimamlaka pamoja na uvaaji unaozingatia maadili kwa watumishi wa umma.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa