Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa wito kwa wananchi wa kata ya Mbigiri kusitisha shughuli zozote za kibinadamu kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza kutokana na shughuli hizo ikiwemo kilimo na shughuli nyinginezo, hivyo kusababisha mto Mkundi kubadili njia yake na kuleta madhara ya mafuriko yaliyopelekea baadhi ya maeneo katika kata hiyo kuharibiwa na maji na kusababisha madhara ikiwemo kuanguka kwa baadhi ya nyumba na wakazi wake kukosa malazi.
Mgoyi amesema hayo Novemba 25 mwaka huu wakati alipowatembelea wananchi wa Mbigiri kwa ajili ya kuwapa pole ambapo amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya shughuli za kibinadamu mto Mkundi umeharibika ambapo hali hiyo imetokana na kutozingatiwa kwa sheria ambayo inasema mita sitini kusiwe na shughuli za kibinadamu lakini kutokana na kutofuatwa kwa sheria hiyo kumesababisha madhara hayo, hivyo shughuli za kibinadamu zisifanyike tena ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.
Pamoja na hayo amesema Mto Mkundi umejaa mchanga na kwamba mto huo unatembe juu ya mchanga na kwamba awali mto huo haukuwa na makazi ya watu wengi lakini kutokana na shughuli za kibinadamu kumekuwa na ongezeko la watu ambao wamekuwa wakiendelea na shughuli za kibinadamu hasa katika kingo za mto jambo lililopelekea madhara yaliyojitokeza na kwamba endapo shughuli za kibinadamu zikiendelea zitaleta madhara makubwa kwani mto huo hauna njia maalum, hivyo kila mwananchi anao wajibu wa kulinda mto huo na kupanda matete ili kuepusha madhara.
Aidha ametoa wito kwa viongozi wote wa serikali za vijiji na watendaji wa kuajiriwa kusimamia sheria ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza kwa wananchi na kwamba kiongozi yoyote atakayeshindwa kusimamia sheria hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, pia amesema ni wajibu wa viongozi na wananchi hao kuwa walinzi wa maeneo hayo kwa kuhakikisha maeneo hayo yanasimamiwa kwa kufuata sheria kwa kutofanya shughuli za kibinadamu kwenye kingo za mto.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amesema kutokana na madhara hayo watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yaliyoathirika wanaendelea na tathmini ili kubaini madhara yaliyojitokeza lengo ikiwa ni kupata kiwango cha madhara yaliyojitokeza kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi lakini pia ametoa rai kwa wananchi wa Mbigiri kuchukua tahadhari ya kutosha kwani mto Mkundi hauna njia moja hivyo ni vyema maeneo hayo yakatumika zaidi kwa ajili ya shuguli za kilimo na kuepuka kuishi katika maeneo hayo kwa kupata makazi mbadala.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa