Wananchi Wilayani Kilosa wametakiwa kuilinda na kuitunza miundombinu mipya ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu itakayowanufaisha wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 3, 2025 na Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta, wakati wa uzinduzi wa kisima cha maji safi katika Shule ya Msingi Kitungu, Kata ya Mtumbatu, ambapo amesema mradi huo umefadhiliwa na Shirika la CAMFED linalojihusisha na kampeni ya elimu kwa mtoto wa kike.
Bi. Beatrice ambaye alikaimu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Elimu kutoka TAMISEMI, Mhe. Atupele Ambwene, ameeleza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha miundombinu inakuwa na usimamizi hivyo amewataka wazazi na walezi kuunda kamati zitakazo simamia visima hivyo na kuhakikisha kushughulikia usafi, uendeshaji, matengenezo na matumizi sahihi ya vyanzo hivyo vya maji.
Pia ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na Taasisi binafsi katika kuleta maendeleo kwa wananchi, hususani kupitia Sekta ya Elimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bi. Beatrice C. Mwinuka amesema Wilaya ya kilosa imekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji na kupelekea kukwamisha shughuli za ujenzi hivyo amewataka wasimamizi wa mradi kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha vijiji vya jirani kupata maji kupitia mradi huo.
Aidha, ameongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya mpango mpana uliohusisha ujenzi wa visima 10 katika shule za Msingi 10 zilizopo katika kata ya Mtumbatu, Mvumi, Mang’ula, Magomeni, Masanze, Mkwatani, Mabwerebwere, Chanzuru, Mamboya na Mbumi.
Naye Mkurugenzi wa CAMFED Tanzania Bi. Nasikiwa Duke amesema kupitia kisima hicho kitasaidia shughuli mbalimbali ikiwemo upandaji miti, upatikanaji wa chakula shuleni lakini pia itaondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Ameongeza kuwa kisima hicho ni cha kisasa kinachotumia mionzi ya jua kuvuta maji chini na kupandisha juu ya vyombo vya kuhifadhia maji ambapo mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 305 hadi kukamilika katika shule zote.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa