Katika kuhakikisha wanafunzi wanapata haki yao ya msingi ya kujifunza katika mazingira bora, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeendelea kuhimiza ushiriki wa jamii, hususani wazazi, katika kuchangia chakula shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mlo wa mchana unaowasaidia kiafya na kielimu.
Wito huo umetolewa Septemba 3, 2025 katika kikao cha kawaida cha utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Bi. Grace L. Nyabange, amezitaka Divisheni na Vitengo zinazohusika na masuala ya lishe ikiwemo Divisheni ya Kilimo, Biashara, Fedha, Elimu Msingi na Sekondari kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha wanayafikia malengo waliojiwekea kuwa kila wanafunzi shuleni anapata chakula bora.
Aidha ametoa msisitizo kwa wazazi kutambua kuwa uchangiaji wa chakula au fedha ni sehemu ya uwekezaji kwa maendeleo ya watoto wao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Daniel Kisoso ameeleza kuwa utoaji wa chakula shuleni umeleta matokeo chanya katika shule nyingi, ikiwa ni pamoja na kupunguza utoro wa wanafunzi na kuongeza ufaulu huku akitoa mfano wa shule zinazotekeleza mpango huo ambazo zimeonyesha mabadiliko makubwa kitaaluma.
Naye Afisa Lishe wa Wilaya, Elisha Kingu, amesema kikao hicho kimekuwa sehemu muhimu ya tathmini na kujifunza kuhusu hali ya lishe wilayani humo. Amesema kuwa kwa robo ya mwisho, kata zote zimefanya vizuri, lakini akasisitiza haja ya idara zote kuendelea kushirikiana ili mafanikio hayo yawe endelevu na kwamba watoto wanapaswa kupatiwa lishe kamili yenye virutubisho muhimu badala ya chakula cha aina moja.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa