Mkuu wa wilaya ya kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia taratibu na sheria zilizopo kuhakikisha haki inatendeka ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao.
Rai hiyo ameitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika 16 Machi, 2024 katika Kitongoji Cha Mbegesela Kijiji cha Ihombwe kata ya Mikumi ambapo Mhe. Shaka amesikiliza kero mbalimbali kama vile mgogoro wa ardhi kati ya Bw. Ndemeka na baadhi ya wananchi katika kitongoji cha Mbegesela.
Akitolea ufafanuzi wa mgogoro huo unaohusisha mwingiliano wa mipaka ambapo Bw. Ndemeka anatuhumiwa kuingia kwenye mipaka ya wananchi wenzake na kujimilikisha ardhi kinyume na sheria , Mhe. Shaka amesema kuwa ni vema kuheshimu sheria, taratibu na maamuzi yaliyokwisha fanywa na viongozi waliopita na si kwenda kinyume kwa kuibua upya migogoro ya miaka ya nyuma ambayo tayari ilishasikilizwa na kutatuliwa na viongozi waliopita badala yake kujikita zaidi katika uzalishaji na kushirikiana katika shughuli za maendeleo.
Ameongeza kuwa ili migogoro ya ardhi iweze kuisha, kila mwananchi anawajibika kumiliki ardhi aliyonayo kisheria ili kuepuka migogoro inayopelekea vitendo vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Pia Mhe. Shaka amewataka wananchi kutoa ushirikiano wao kwa jeshi la polisi kwa yeyote anayekwenda kinyume na sheria na kusababisha vitendo vya uvunjivu wa amani sheria kali zichukuliwe ikawe fundisho kwa wengine.
Sambamba na hayo Mhe. shaka ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia kata ya Mikumi fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.28 kwa ajili ya Ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo Daraja na shule ya Sekondari.
Pia amempongeza mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Dennis Londo kwa juhudi zake za kuleta mnara wa Mfilisi ambao ukikamilika utatua changamoto ya mawasiliano katika kata hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa