Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewataka Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji waliochaguliwa 27, Novemba 2024 kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya kuwaongoza wananchi ikiwa ni pamoja na kujiepusha na michango inayowakandamiza wananchi.
Mhe. Shaka ameyasema hayo 16 Disemba, 2024 akiwa ni mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wenyeviti hao yaliyofanyika katika Tarafa ya Magole.
Aidha Mhe. Shaka amewata kuitumia vizuri dhamana waliyopewa na wananchi na kuwataka kuacha mara moja kuchangisha michango isiyo na tija kwani imekuwa ni changamoto kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kutoa michango hiyo.
Sambamba na hayo, pia amewaasa viongozi hao kuhakikisha kuwa wanapoitisha mikutano ya Vijiji au Vitongoji wahakikishe kuwa wanawasomea wananchi mapato na matumizi ili kuondoa malalamiko kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Viongozi hao walioingia madarakani wajitahidi kuepukana na kutoshiriki kuwa chanzo cha migogoro ya wakulima na wafugaji na badala yake wawe mstari wa mbele kuhakikisha wanatenda haki kwa pande zote mbili ili kuepusha migogoro hiyo iliyopo ndani ya Wilaya ya Kilosa.
Kwa Upande wake Mratibu wa mafunzo hayo, Mhadhili Mwandamizi kutoka Chuo cha Hombolo Dkt. Michael Msendekula amesema kuwa kupitia mafunzo hayo ya siku mbili washiriki watapata uelewa kupitia mada mbalimbali kama vile sheria zinazohusiana na serikali za mitaa, mikutano na vikao katika mamlaka ya serikali za mitaa, Muundo, mfumo pamoja na majukumu yao kama wenyeviti wa vijiji na wenyeviti wa vitongoji, Usimamizi wa miradi na pia namna bora ya kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Aidha kwa Upande wake Afisa Uchunguzi kutoka Ofisi ya Takukuru Wilaya ya Kilosa Bwana Emiri Okelo amesema kuwa Viongozi hao wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa huku akiwataka kutenda haki ili kuepukana na madhara ya kutoa au kupokea rushwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa