Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka H Shaka ametoa rai kwa watumishi kuendelea kuchapa kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kila mmoja katika eneo lake msisitizo ukiwa katika kujenga umoja na ushirikano ili kuwa na mwelekeo wa kuleta maendeleo na tija ndani ya wilaya jambo litakalosaidia kuondoa dhana potofu iliyopo miongoni mwa baadhi watu kuwa Kilosa ni wilaya ya migogoro.
Rai hiyo ameitoa Februari 28 mwaka huu katika kikao chake na watumishi ambapo amesema kuwa ili kuwa na kilosa isiyo na migogoro ni lazima kushirikiana na kuendana na falsafa ya Uongozi wa Pamoja kwa Maendeleo Endelevu ambapo ili kuwa na maendeleo, lazima kuwa na viongozi na watumishi ambao wana nia moja ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuwaletea maendeleo wananchi kwa kila mmoja kuwajibika ipasavyo katika eneo lake.
Shaka amesema kuwa Kilosa kuwa na maendeleo endelevu ni hakika na inawezekana, kwani ina fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uwepo wa reli ya mwendokasi(SGR) ambayo inatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu na kwamba kupitia uzinduzi wa reli hiyo utapelekea uwepo wa fursa mbalimbali za kiuchumi ambapo ili kufikia tija hiyo lazima Wilaya itumie muda mwingi kujadili maendeleo, kwa kuhakikisha inajiweka vizuri katika masuala mbali ya ardhi, uchumi, huduma za kijamii, utawala bora na masuala ya uwekezaji.
Aidha amesema kuwa katika uongozi wake hatakubali kumvumilia kiongozi asiye mwadilifu na kuwa chanzo cha migogoro kwa kuendekeza rushwa bali kila mmoja ahakikishe anafuata sheria, kanuni na taratibu na kuzingatia maadili, huku akisisitiza kuwepo kwa juhudi za makusudi katika kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, ambapo ametaka fedha yoyote inayokusanywa kupelekewa benki kama zilivyo taratibu badala ya kuanza kuzitumia bila kufuata utaratibu.
Naye Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila amewaomba watumishi wote wa wilaya ya Kilosa kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kiongozi huyo, hususani katika utekelezaji wa majukumu ili kuiletea Kilosa maendeleo na kwamba ili kufanikisha hilo kila mmoja anapaswa kuwajibika ipasavyo katika eneo lake kwa kuzingatia nidhamu, uaminifu, uadilifu na maadili ya kiutumishi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa