Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewataka viongozi kwa nafasi za uteuzi na waliopangiwa majukukumu ya kiutendaji katika taasisi za umma kuchunga dhamana waliyopewa na serikali kwa kuwa waadilifu.
Mhe. Shaka ametoa wito huo 03 Februari 2025 wakati akitoa hotuba yake kwenye maadhimisho ya kilele cha siku ya Sheria Nchini ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za kimahakama Nchini yaliyofanyika katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa.
Mhe. Shaka ameongeza kuwa serikali inapotoa teuzi ya Jaji au Hakimu kwenye utumishi wa umma haina maana ya kwamba wamepewa kibali cha kuumiza wengine ama kutengeneza mianya ya kujitajirisha kimaslahi isipokuwa wanatakiwa wawe na dhana ya uadilifu, uwazi na uaminifu.
“Rushwa ni kiashiria kimoja wapo cha ukwamishaji wa maendeleo ndani ya Wilaya yetu”. Alisema Mhe. Shaka
Aidha Mhe. Shaka amesema kuwa kila kosa lihukumiwe kwa mujibu wa taratibu za kisheria na matakwa ya katiba ya nchi bila mwananchi yeyote kuonewa.
Pia Mhe.Shaka ameishukuru na kuipongeza Mahakama ya Wilaya kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kurudisha imani, sura na uhalisia wa Mahakama kwa wananchi ambapo malalamiko mengi hususani upande wa migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua kwa kiasi kikubwa.
Sambamba na hayo Mhe. Shaka amesema serikali ya wilaya ya Kilosa itasimamia mambo tisa yaliyoshauriwa kufanyika katika kuboresha mfumo wa haki na madai nchini ili kupunguza migogoro ikiwemo kuanzishwa kwa mabaraza vijijni yatakayosimamiwa na wazee wa mila, uwepo na utekelezaji wa sheria ndogo ndogo za halmashauri, kuhamasisha usuluhishi wa migogoro kama njia mbadala ya kutatua kesi kwa haraka na gharama nafuu kabla na baada ya kufunguliwa mahakamani.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa