Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewataka Viongozi ngazi ya kata na vijiji kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta maendeleo katika maeneo yao pasipo kutanguliza maslahi binafsi kwani kwa kufanya hivyo kutakwamisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Mhe. Shaka ameyasema hayo Juni 30, 2025 kwenye kikao cha kutoa tathmini ya uvunaji wa mazao ya misitu ndani ya Wilaya ya kilosa chenye lengo la kujadili na kuwapitisha waombaji wapya wa uvunaji wa mazao ya misitu kwa mwaka mpya wa fedha 2025/2026 ambapo Mhe. Shaka amesema kuwa viongozi wamepewa dhamana ya kulinda na kutetea maslahi ya wananchi.
Mkuu huyo wa Wilaya amewasisitiza viongozi hao kutimiza majukumu yao ipasavyo pasipo kujihusisha na vitendo vya rushwa au upendeleo kwa baadhi ya watu na badala yake wasimamie haki, sheria, kanuni na taratibu zilizopo .
Kwa upande wake Mhifadhi Misitu Wilaya Bi. Hilda R. Mwalongo amesema kuwa masuala ya uvunaji yana umuhimu kwasababu yanasaidia katika ukusanyaji wa mapato ya Vijiji na Serikali kwa ujumla ambapo uvunaji huo ni endelevu na unafuata mipango inayosimamiwa kwa utaratibu uliopangwa ili kusaidia uvunaji wenye tija wa mazao hayo ikiwemo magogo, kuni na mkaa.
Hilda ameongeza kuwa Halmashauri kwa kushirikiana na Wakala wa Uhifadhi wa misitu Tanzania (TFS) inajukumu la kuelimisha jamii hasa wakati huu wa kuelekea msimu wa kiangazi wa kuandaa mashamba kufuata taratibu na miongozo ya uvunaji ili kuondoa uharibifu wa mazao ambapo jamii imekuwa ikijihusisha na ukataji wa mapori holela unaosababishwa na ongezeko la watu pamoja na uhitaji wa mashamba kwa ajili ya kilimo.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Chabima Julius Magungu amesema kikao hiko kimewajengea uwezo na uelewa wa umuhimu wa utunzaji wa misitu katika maeneo yao wanayoyawasimamia ili kupunguza uharibifu wa ukataji wa misitu kiholela ambapo wamefanya matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uvunaji wa mazao ya misitu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa