Mkuu wa wilaya ya kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewataka walanguzi na wafanyabiashara ya sukari kufuata bei elekezi iliyopangwa na serikali ili kuweka usawa kwa wananchi wote kupata bidhaa hiyo muhimu.
Mhe. Shaka ameyasema hayo Februari 22, 2024 katika kikao cha Baraza la Ushauri Wilaya (DCC) kilichofanyika katika ukumbi wa FDC Ilonga ambapo amesema hatua kali za kisheria zitafuatwa endapo wafanyabiashara hao watakiuka tamko la serikali.
Mhe.Shaka amewataka wananchi kutoa ushirikiano wao kwa jeshi la polisi pamoja na kamati ya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kwa wakati endapo watabaini kuna wafanyabiashara wanaokiuka kufuata bei hiyo elekezi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Ameongeza kuwa kamati ya ulinzi na usalama inaendelea kufatilia suala hilo kwa ukaribu mkubwa ambapo wamefanya ziara ya kutembelea maduka katika maeneo mbalimbali kuona mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo pamoja na kufanya ziara ya kutembelea kiwanda cha sukari cha Mkulazi ambacho kinaendelea na uzalishaji wa sukari pamoja na changamoto zilizopo katika mashamba ya miwa kujaa maji kutokana na mvua zilizonyesha na kusababisha mazingira kutokuwa rafiki katika mashamba hayo.
Sambamba na hayo ameeleza kuwa kamati ya ulinzi na usalama imefikia maamuzi ya pamoja na kiwanda cha sukari cha Mkulanzi kwa kuwatumia mawakala wa usambazaji wa sukari katika ukanda wa kilosa na kipaumbele cha kwanza ni wananchi wa kilosa kusambaziwa sukari hasa katika maeneo ya dumila, kilosa kati, ulaya na maeneo jirani.
Aidha Mhe. Shaka ameongeza kuwa kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kusaidiana kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo kwa mwaka 2023 hakuna vifo vilivyosababishwa na migogoro ya wakulima na wafugaji ukilinganisha na miaka nyuma. Sambamba na kutatua migogoro ya ardhi kwa kuandaa program maalum ya kuelimisha wananchi juu ya kumiliki ardhi kisheria.
Kwa upande mwingine amewasisitiza Watumishi wa Halmashauri kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ili kuweza kuwasaidia viongozi kutekeleza mipango inayopangwa katika kuwaletea Wanachi maendeleo,Pia amemshukuru Rais wa Tanzania Mhe Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi kwaajili ya utekelezaji wa Miradi ya maendeleo Wilayani hapa.
Akizungumza juu ya bajeti Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael J.Gwimile amesema kuwa amepokea ushauri na maoni kutoka kwa wajumbe mbalimbali wa baraza la ushauriWilaya na kusema kuwa wataalam wataendelea kufanya marekebisho katika bajeti kulingana na maoni na ushauri ulivyotolewa .
Pia katika suala la ujenzi wa vituo vya Polisi Gwimile ameshauri wananchi wahamasishwe kuchangia ujenzi vituo vya polisi kama ambavyo wanafanya katika miradi mingine ya maendeleo kwani suala la usalama ni muhimu kwa mustakabali wa Kilosa nzima pia ameongeza kuwa halmashauri inaweza kuongeza nguvu kwa kutenga bajeti kutoka mapato ya ndani ili kumalizia ujenzi wa vituo vya polisi ili kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa