Wananchi ya Kijiji cha Maguha wamemuomba mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka kutatua kero zao ikiwepo migogoro ya mashamba pamoja kumaliza mipasuko iliyoko baina ya viongozi wa Kijiji na wajumbe wa kamati ya Halmashauri ya kijiji hicho.
Wameyasema hayo katika mkutano ulioandaliwa na mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ikiwa na lengo la kusikiliza kero za wananchi ambao umefanyika Disemba 20, 2023 katika Kijiji ch Maguha ambapo mkuu wa Wilaya ameambata na vyombo vya ulinzi na usalama na kamati kuu ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilosa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti, wanakijiji wameainisha kuwa baadhi ya miradi ya maendeleo kama vile Zahanati ya Kijiji na Shule ya Msingi Maguha miundombinu yake haijakamilika ikiwemo miundombinu ya umeme katika Zahanati hiyo.
Aidha kero nyingine iliyoainishwa ni wizi wa mali za serikali yakiwemo mabati lakini pia suala la migogoro ya wakulima na wafugaji ilitajwa kuwa ni kero ya muda mrefu.
Kwa upande wa wafugaji wakiwakilishwa na bwana Mnyogi Mhando wameiomba serikali kufikisha huduma ya maji katika makazi yao kwani husafiri kwa umbali mrefu kufuata huduma hiyo lakini pia wamewaomba wakulima kutojuchukua sheria mkononi ikiwa ni pamoja na kuchoma pikipiki zao pale unapotokea mzozo kati ya wakulima na wafugaji.
Hata hivyo, viongozi na wataalamu mbalimbali wakiwemo diwani wa kata ya Maguha bwana Andrea Chaunga, Mtendaji wa Kata ya Maguha bwana Sembuli Mwegalawa, Mtendaji wa kijiji cha Maguha bwana Keneth Mazoba, Mwenyekiti wa Kijiji hicho bwana Fransis Sekwao pamoja na wataalumu kutoka ngazi ya wilaya walipewa nafasi ya kujibu kero zilizowagusa moja kwa moja.
Akitolea ufafanuzi kuhusu utaratibu wa matumizi ya pesa za kiserikali katika akaunti za benki, Mwakilishi wa Mkurugenzi bwana Hussein Ayoub ambaye ni Afisa Utumishi amesema kuwa serikali imeweka utaratibu ambapo fedha hizo hutolewa kwa mfumo wa FAS ambapo Halmashauri ya kijiji hukaa na kupanga matumizi ya fedha zilizopo kisha mkutano mkuu na baada ya hapo hupelekwa kwenye kitengo cha ukaguzi na fedha cha halmashauri ya wilaya ili kuwekewa vifungu vya matumizi ya fedha hizo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilosa bwana Shabani Mdoe amewataka viongozi wa serikali ya kijiji hasa wajumbe wa halmashauri ya kijiji kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuwataka waoneshe ushirikiano kwa watendaji wa serikali ili kuleta maendeleo ya kijiji hicho kama Ilani ya chama hicho unavyotaka.
Akiitimisha mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkoni bali wafuate taratibu za kisheria ili kupata haki yao. Ameongeza kuwa serikali haitasita kumchukulia hatua za kisheria mwananchi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa