Wananchi ndani na nje ya Wilaya ya Kilosa wametakiwa kutumia fursa za uwekezaji zilizopo Wilayani humo ili kuhakikisha uchumi unaimarika na kuleta maendeleo.
Wito huo umetolewa Juni 30, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka katika mkutano wa Baraza la biashara uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na kusema kuwa zipo fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo Utalii, Kilimo, Mazingira, Madini na Viwanda.
Mhe. Shaka ameeleza kuwa ili kuunga mkono jitihada za serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wadau wa sekta binafsi wanatakiwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Kilosa na kutumia fursa zilizopo ndani ya Wilaya ili kuimarisha uchumi na kuchochea ustawi wa maendeleo katika jamii.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Wilaya ya Kilosa Bw. Edward Mapile amesema kuwa baraza hilo limefanyika ili kutoa fursa kwa sekta binafsi na Serikali kupeana taarifa mbalimbali za maendeleo na kutatua changamoto zinazojitokeza na kufanya marekebisho yatakayopelekea kuongeza maendeleo katika Wilaya ya Kilosa.
Mapile ameongeza kwa kusema kuwa kwa sasa Wilayani Kilosa zipo fursa mbalimbali kama vile uwepo wa reli ya SGR inayorahisisha usafiri na kuongeza kasi ya uwekezaji kwa wadau wa sekta binafsi hivyo amewasihi wajitokeze kuwekeza ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa