Wananchi wa Kata ya Uleling’ombe wametakiwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa bweni la wasichana la Shule ya Sekondari Uleling’ombe, kwa kujitolea nguvu kazi na rasilimali ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Septemba 14, 2025, uliolenga kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika eneo hilo.
Amesema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya elimu, hasa kwa mtoto wa kike ambaye mara nyingi hukabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira.
Mradi wa ujenzi wa bweni hilo umefadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa gharama ya shilingi milioni 154, ambapo ukikamilika unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi wa kike.
Aidha, mradi huo unatakiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2025 kama ilivyopangwa, huku akiwahimiza wazazi na viongozi wa kijamii kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha watoto wao wanapata fursa ya elimu katika mazingira bora, salama na rafiki kwa mtoto wa kike.
Kukamilika kwa bweni hilo kutasaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, hali ambayo imekuwa ikichangia utoro na matokeo duni kwa baadhi ya wanafunzi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa