Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewataka Wafugaji Wilayani humo kuhakikisha mifugo yote inachanjwa ili kusaidia kudhibiti mifugo hiyo kupatwa na magonjwa mbalimbali.
Mhe. Shaka ameyasema hayo Julai 30, 2025 katika Uzinduzi wa Kampeni ya chanjo za ruzuku na Utambuzi wa Mifugo uliofanyika Kiwilaya katika Kijiji Cha Kiduhi Kata ya Kilangali na kusema kuwa utoaji wa chanjo hizo utaongeza Thamani ya mifugo.
Mhe. Shaka ameongeza kwa kuwataka wataalamu wafuate utaratibu wa kazi na pia watoe mafunzo ili kuwaelimisha wafugaji ambao bado hawajapata elimu juu ya faida ya zoezi hilo.
Aidha amesema kuwa zoezi hilo litasaidia kutambua mifugo na kutunza takwimu ambazo zitasaidia kuepusha kuingiza na kutoa mifugo kiholela ndani ya Wilaya hivyo kuepusha Migogoro.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bi. Beatrice Mwinuka amesema kuwa zaidi ya dozi laki tano zimeandaliwa kwa ajili ya zoezi hilo ambapo amezitaja kuwa ni pamoja na chanjo ya magonjwa ya homa ya mapafu kwa Ng’ombe,Sotoka ya Mbuzi na Kondoo,na Chanjo ya kuku dhidi ya magonjwa ya mdondo, mafua na Ndui.
Bi. Mwinuka ameongeza kwa kusema kuwa mpango huo wa utoaji chanjo ni wa miaka mitano ambao umeanza mwaka 2025 hadi 2029 na maandalizi yote yamekamilika hivyo amewaasa Wafugaji kupeleka mifugo yao ikapatiwe chanjo katika maeneo maalumu yaliyoandaliwa kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake Chifu wa Kabila la kimasai Ndg. Matayane Simanga amesema kuwa wao kama wafugaji wamepokea vizuri zoezi hilo la chanjo na utambuzi wa mifugo na wapo tayari kushirikiana kikamilifu na wataalamu wanaohusika na huku akiwatoa hofu wafugaji kwa kusema kuwa chanjo hizo ni salama na wala hazina madhara yeyote kwa mifugo .
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa