Waheshimiwa Mahakimu wa Mahakama za Wilaya ya Kilosa wametakiwa kutenda haki pindi wanapotoa uwamuzi katika masahauri ya kesi mbalimbali ili kulinda na kusimamia utawala wa kisheria ikiwemo kuondoa migogoro kwa wananchi bila ubaguzi wowote.
Kauli hiyo imetolewa Februari Mosi, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka wakati akitoa hotuba yake katika maadhimisho ya sheria nchini yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Wilayani hapo.
DC shaka amesema kuwa ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakidai kutotendewa haki katika maamuzi yanayotolewa katika mahakama hizo na kupelekea ofisi yake kuanza kusikiliza kero hizo ambapo amewataka mahakimu hao kuzingatia kauli mbiu yam waka huu isemayo “Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa taifa nafasi ya mahakama na wadau katika kuboresha mfumo junuishi wa haki jinai”.
Ameongeza kuwa Mahakama ni muhimili katika serikali hivyo wanapaswa kushirikiana na wadau wa sheria kutekeleza dhana ya kauli mbiu hiyo kwa kuwajibika, kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa ili kujiepusha na rushwa na mwenendo ambao sio wa maadili kwani changamoto za kesi za migogoro ya ardhi kwa wakulima na wafugaji zimekuwa hazitendewi haki .
Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhasisi dhana ya haki jinai hivyo wadau wa sheria na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama waendelee kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia haki.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa Agnes Ringo amesema tangu kuadhimishwa kwa maadhimisho hayo mwaka 1966 yamekuwa chachu kwa maboresho ya mahakama na wananchi ambapo kabla ya kufikia kilele cha maadhimisho hayo mahakama iliweza kutoa elimu ya kisheria maeneo mbalimbali kuanzia tarehe 24 hadi 30 Januari, 2024.
Amesema Mahakama ya Tanzania ina jukumu ya haki kwa watu wote pasipo ubaguzi ambapo katika utekeleza kwa vitendo imekuwa ikifanya maboresho katika utendaji kazi wake ambapo Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu huo Januari,2023 aliteua tume ya haki jinai ikitoa pendekezo la kuboreshwa kwa mahakama na wadau katika haki jinai ili haki ionekane imetendeka kwa wakati.
Sambamba na hayo Mhe. Ringo ameongeza kuwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na amani mahakama na wadau wana umuhimu kushirikiana katika mfumo jumuishi wa haki jinai kwani maendeleo ya taifa yanategemea uwepo wa amani.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa