Watendaji wa Uboreshaji ngazi ya Jimbo wametakiwa kuzingatia mafunzo waliyoyapata ili kufanikisha zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura linalotarajia kuanza tarehe 01 hadi 07 Machi, 2025 katika Jimbo ya Kilosa na Mikumi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Beatrice Mwinuka wakati akizungumza na watendaji hao katika semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo iliyofanyika tarehe 22- 23 Machi, 2025 katika ukumbi wa chuo cha Ualimu Ilonga
Bi. Mwinuka amesema kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na serikali kwa ujumla inategema utendaji kazi bora wa watendaji hao katika kufanikisha zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kwani zoezi hilo ndilo litakalotoa dira kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba, 2025.
Aidha amewataka watendaji hao kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na kuwasihi kuendelea kuwasiliana kwa karibu na mamlaka husika pale inapotokea changamoto yoyote.
Akifunga mafunzo hayo Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Mikumi na Kilosa Ndg. Betuely Ruhega amewapongeza watendaji hao kwa kuaminiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia Uandikishaji huo huku akiwataka kufuata miongozo na mafunzo waliyoyapa ili kufanikisha Uboreshaji huo.
Katika hatua nyingine, amewakumbusha kuzingatia kiapo walichoapa lakini pia maadili ya kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa lakini pia kutunza vifaa watakavyokabidhiwa kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Akitoa salamu za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mjumbe wa INEC Ndg. Francis Sang’wa amewataka watendaji hao kuhakikisha wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha, wanajiandikisha ili wapate haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa