Misitu ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi ambayo inahitaji ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha inakuwa endelevu hivyo ipo haja ya jamii kushirikishwa kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha inatunzwa na kutumika katika hali uendelevu ili kuleta matokeo chanya.
Hayo yamebainishwa na Meneja mradi wa TTCS Bw. Charles Leonard ambapo amesema Tanzania ina hekta 48.1 za misitu hivyo ni vema ikatumika nguvu ya ziada kwa jamii katika kuielemisha na kujenga uelewa namna ya kuhifadhi, kutunza na kutumia misitu katika hali ya uendelevu kwani jamii ikielimika na kupata uelewa mtazamo wao utabadilika kuhusu kulinda, kutunza na kutumia rasilimali misitu.
Leonard amesema kuwa misitu inaweza ikawa endelevu endapo jamii itashiriki kwa kulinda misitu dhidi ya shughuli haribifu za kibinadamu, na kwamba usimamizi shirikishi ni fursa ya maendeleo endelevu ambayo inapunguza uharibifu wa misitu lakini pia inaongeza motisha kwa wananchi na vijiji, Serikali na Halmashauri zinafaidika kwa kupata mapato hivyo ni vema kuendelea kutanua wigo wa kutunza misitu katika njia shirikishi.
Aidha kwa upande wa Maafisa Habari na Mawasiliano kutoka serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali walioshiriki ziara ya kujenga uelewa juu ya mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) wamesema mradi huo umetekeleza dhana ya uendelevu wa misitu ya vijiji na kulinda mazingira ambapo mkoani Morogoro unatekelezwa katika wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro katika vijiji 35 huku wakisema kuwa ipo haja ya mradi huo kufanyika na kuendelezwa nchi nzima kwani una manufaa kwa nchi na wananchi kiujumla.
Pamoja na hayo wamesema mradi huo unachochea utunzwaji wa mazingira na kuinua kipato cha wananchi huku wakisema kuwa endapo Serikali kwakushirikiana na wananchi watatunza misitu hiyo itasaidia katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, upatikanaji wa madawati na mbao kwa matumizi mbalimbali jambo litakalosaidia kuepusha matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa rasilimali za misitu kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Akitoa taarifa fupi ya faida ya mradi wa Mkaa endelevu katika kijiji cha Kitunduweta Afisa Mtendaji wa Kijiji Bw.Thomas Lukoo amesema, “Kijiji cha Kitunduweta kwa mwaka kinavuna vitalu 83 sawa na gunia 6,640 ambapo kwa mwaka wa kwanza walipata Tsh. 28,328,095/=, mwaka 2018/2019 walipata Tsh. 27,128,095/= na mwaka 2019/2020 Tsh. 28,143,255/= lakini wameweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kama kuwakatia wananchi Bima ya Afya ya CHF takribani kaya 378, pia wamefanya ukarabati wa madarasa ya shule ya msingi Kitunduweta, wamemalizia nyumba ya mwalimu mkuu pamoja na kujenga choo cha kisasa cha nyumba ya mwalimu na pia wametengeneza madawati kwa ajili ya shule yao.
Naye Mratibu wa Mradi wa Mkaa Endelevu upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambaye pia ni Afisa Maliasili Bw. John Mtimbanjayi amesema yapo mafanikio yaliyopatikana baada ya mpango wa usimamizi shirikishi ikiwemo kupungua kwa hali ya uharibifu wa misitu kwa kiasi kikubwa kwani vijiji vinapata fursa ya kupata uelewa namna ya kutunza misitu hiyo lakini pia vinapata fedha zitokanazo na ushuru wa mazao ya misitu, fedha ambazo zinasaidia shughuli za maendeleo kwenye vijiji husika huku akieleza changamoto inayojitokeza kutokana na uwepo wa kanuni ya mapendekezo ya bei ya mazao ya misitu GN417 hususani katika zao la mkaa kuwa na bei ilekezi ya shilingi 12500 kwa gunia la kilo 50 ambapo awali ilikuwa 6750 hivyo kupelekea wateja wengi kununua mkaa maeneo ya mijini badala ya kununua maeneo ya vijijini ili kuepuka gharama za usafirishaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa