Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa wito kwa wakulima na wafugaji kuhakikisha msimu huu wa mavuno unapita kwa usalama pasipo migogoro ambayo husababisha mapigano baina ya wakulima na wafugaji na kusababisha athari mbalimbali ikiwemo vifo na upotevu mazao jambo litakalosababisha uwepo wa amani nyakati zote na majira yote na kwamba matatizo ya Kilosa yanatatuliwa na wanakilosa wenyewe.
Mkuu wa Wilaya amesema kuwa athari ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa miaka ya nyuma kwa asilimia kubwa kwa mwaka 2017 zilipungua kutokana na ushirikiano ulioonyeshwa baina ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Kamati ya Amani Wilaya, wakulima na wagufaji hivyo kwa mwaka huu wa 2018 anatoa rai kwa wote kuongeza juhudi za kudumisha amani ili hali ya mapigano isijitokeze tena.
Sambamba na hayo amewataka wafugaji kumiliki mifugo wanayoweza kuimudu pamoja na kuacha mara moja tabia ya kuwaachia watoto mifugo kwani watoto hawana uwezo wa kuilinda, hivyo kusababisha mifugo kuingia mashambani na kula mazao ya wakulima, na amebainisha kwamba atakayebainika kuwaachia watoto mifugo Kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wa tarafa na kata watakamata mifugo pamoja na wahusika kisha kuwashughulikia kisheria ikiwemo kushtakiwa kwa kukiuka sheria ya mwaka 1978 inayowalinda watoto na kutaka wasinyimwe haki zao za msingi ikiwemo haki ya kupata elimu.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kessy Mkambala amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na miongozo ikiwemo kufanyika kwa mikutano na vikao vya mara kwa mara ili kujadili maendeleo ya maeneo yao pamoja na kutatua changamoto zinazojitokeza ama kuwakabili.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa