Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amewataka viongozi wa tarafa, kata na vijiji pamoja na kamati za amani zilizoko katika kata na vijiji kukaa kwa pamoja kuweka mikakati ya pamoja ya kudumisha amani ana utulivu ambayo imeanza kupotea kutokana na migogoro mbalimbali ambayo imeanza kujitokeza.
Mgoyi ametoa maagizo hayo Juni 24 mwaka huu katika kikao chake na maafisa tarafa, wajumbe wa kamati ya amani Wilaya pamoja na watendaji wa kata na kusema kuwa kila mmoja atimize wajibu wake kwa kuhakikisha amani inapatikana kwa kubainisha vyanzo vya migogoro na kuitafutia suluhu jambo litakalosaidia kuwepo kwa amani huku akitaka kusimamiwa kwa sheria ndogo ndogo na kuhakikisha zinafanya kazi lakini pia kuhuishwa kwa kamati za amani huku akiagiza kukamatwa mara moja kwa wafugaji waliobainishwa kuwa ni wakorofi na kutotii sheria.
Nao wajumbe walioshiriki kikao hicho wamebainisha vyanzo mbalimbali vya migogoro hiyo ikiwemo hulka ya kuhama hama kwa wafugaji ili kutafuta malisho, uuzaji wa mabua mashambani, mifugo kuingizwa mashambani pamoja, tabia ya uongo inayojitokeza hususani zinapofanyika tathmini zisizo sahihi pamoja na umiliki wa mashamba feki baina ya wakulima.
Pamoja na hayo viongozi wa dini walioshiriki kikao hicho wamewasihi viongozi hao kwa ngazi ya tarafa, kata na vijiji kuendelea kudumisha amani na utulivu hususani kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu huku wakitaka kukemewa kwa dhambi ya unafiki bali watu wawe wa kweli na kutenda haki.
Wakati huo huo Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila amesisitiza suala zima la uwajibikaji na uadilifu huku akisema kuwa wajibu wa kwanza wa viongozi hao ni kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu katika maeneo yao kwani asilimia kubwa ya migogoro hutokana na kukosa uadilifu lakini pia ametaka kuchukuliwa kwa hatua stahiki mapema kwa wale wote wanaosababisha uvunjifu wa amani badala ya kusubiri tatizo liwe kubwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa