Kilosa yaadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika na 59 ya Jamhuri kwa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kiasi cha fedha shilingi bilioni 4.3 zilizotolewa na Serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi sambamba na kuendelea kutatua changamoto ya maji kwa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh. Majid H. Mwanga wakati wa maadhimisgho hayo kiwilaya ambapo amesema Serikali imeitupia jicho la tatu Wilaya ya Kilosa kwa kiasi hicho cha fedha ambazo zinawezesha ujenzi wa vyumba 186 vya madarasa kwa shule za sekondari na shule shikizi kwa elimu msingi, ununuzi wa mashine ya mionzi, vyumba vya wagonjwa mahututi na nyumba za watumishi.
Akizungumzia suala la usafi wa mazingira Mwanga amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru na 59 ya Jamhuri kila mmoja aadhimishe kwa kufanya usafi katika eneo lake la makazi, biashara na ofisi lengo ikiwa ni kuifanya Kilosa kuwa katika muonekano safi na kwamba Mkuu wa Wilaya atatembelea maeneo mbalimbali ili kukagua na yeyote ambaye hatotimiza agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake huku akisisitiza suala la kufanya mazoezi kwa ajili ya kuboresha afya ambapo amesema kwa upande wa Kilosa mazoezi hufanyika kila siku za Jumamosi na Jumapili asubuhi, hivyo anawakaribisha wananchi wote kushiriki mazoezi hayo.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya Shaban Mdoe amepongeza wajasiriamali walioshiriki katika maadhimisho hayo kwa kuonyesha bidhaa wanazofanya ambapo pia amesisitiza urejeshwaji wa mikopo kwa wakati ili vikundi vingine viweze kukopa huku akitoa rai kwa wananchi kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa Serikali ili kuipa Kilosa maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba ameshukuru Serikali kwa namna inavyowaletea maendeleo wananchi ambapo amesema kwa sasa ujenzi wa vyumba vya madarasa unaendelea vizuri katika kata mbalimbali ambapo pia amepongeza wanafunzi walioshiriki katika mashindano ya uandishi wa insha kwa shule za msingi na sekondari ikiwa ni sehemu ya kuchagiza maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru na 59 ya Jamhuri.
Wilaya ya Kilosa imefanya maadhimisho hayo kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha jamii kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo mbalimbali, kuwashindanisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika mashindano ya uandishi wa insha na wajasiriamali kuonyesha bidhaa zao ambapo washindi walitangazwa na kupongezwa kwa juhudi zao walizozionyesha.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa