Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. William Tate Ole Nasha ametoa wito kwa walimu wote nchini kuwa wazalendo kwa nchi yao na kuongeza juhudi katika kuendeleza taifa letu hasa katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanaowafundisha pindi wanapokua mashuleni wanakuwa wazalendo na kuienzi nchi yao katika kudumisha mema nchini.
Naibu Waziri huyo ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Chuo Cha Ualimu Ilonga na Chuo cha Ualimu Dakawa vyote vya wilayani Kilosa na kusema kuwa ukitaka kujenga uzalendo kwa watu ni lazima ujenge kwanza kwa walimu kwani walimu ni watu ambao kila mwananchi mwenye kada yoyote lazima apite kwenye mikono ya mwalimu, hivyo walimu wote nchini wanapaswa kuheshimu na kuthamini uzalendo kwani walimu wasipokuwa wazalendo hawawezi kufundisha watoto watakaokuwa wazalendo wenye kuipenda nchi yao, na kuongeza kuwa ili walimu hao tarajali wawe mahiri wanapaswa kuwa makini hasa katika elimu na masuala ya TEHAMA, na kwa sababu hiyo vyuo vyote vya ualimu vitaunganishwa katika mfumo wa TEHAMA ili kuweza kuendana na mkazo uliopo wa maarifa na uwezo wa mwanafunzi kuweza kujitegemea na kuwa wabunifu wanaoweza kutengeneza fursa za maendeleo kupitia mifumo mbalimbali kwani Taifa, Serikali na jamii kiujumla inawategemea zaidi walimu.
Akijibu changamoto mbalimbali zilizowasilishwa kwake na wakuu wa vyuo vya Dakawa na Ilonga amesema serikali imenunua magari 35 kwa ajili ya vyuo vyote 35 nchini ambapo magari mawili yataletwa katika vyuo hivyo, na kwamba chuo cha Dakawa kitapatiwa kompyuta 30 kwa ajili ya kuendana na kasi ya ujifunzaji huku akiahidi changamoto ya mawasiliano inayovikumba vyuo hivyo kupatiwa ufumbuzi kwa kufanya mawasiliano na watu wa mawasilano ili kutatua changamoto hiyo.
Sambamba na hayo amesema kuwa taratibu zinaendelea ili kuhakikisha vifaa vya maabara vinapatikana vyuoni, na kwamba serikali inaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya ujifunzaji na kufundishia kwa kuhakikisha miundombinu inarekebisha ikiwemo ukarabati wa majengo mbalimbali vyuoni ili kuhakikisha wanachuo wanaishi katika mazingira rafiki.
Akizungumzia hali ya elimu Naibu Waziri amesema licha ya jitihada zinazofanyika bado hali si ya kuridhisha, hivyo amemuagiza Mdhibiti Ubora Elimu wa Kanda na Afisa Elimu Mkoa kukaa na uongozi wa wilaya kuona nini kifanyike ili kupandisha kiwango cha ufaulu licha ya changamoto mbalimbali zinazosababisha ufaulu kutokuwa wa kuridhisha ikiwemo sababu za kijiografia.
Ole Nasha amesema serikali iko bega kwa bega na walimu na kwa kutambua umuhimu wao katika jamii serikali itaboresha maslahi ya walimu, na amewataka walimu hao tarajali kutambua kuwa bado kuna ongezeko la watu, hivyo serikali inaendelea kuhitaji shule na walimu na kwamba miaka michache iliyopita watu wasiokuwa na sifa walikua wakiajiriwa na kusababisha wenye sifa kukosa ajira jambo ambalo kwa sasa serikali imelidhibiti, hivyo waongeze bidii katika masomo na suala la ajira waiachie serikali ambapo kwa mwaka huu imeajiri walimu 6000.
Naye mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam I. Mgoyi ametoa ombi kwa Naibu Waziri kuangalia ka jicho la tatu eneo lililopo katika chuo cha Dakaa kwani ni eneo linalofaa kwa matumizi mengine ikiwemo kuanzisha chuo kikuu katika eneo hilo pamoja na kuangalia namna ya kutenga fedha ambazo zitatumika kukarabati miundombinu iliyopo eneo hilo ambayo kwa sasa ni chakavu, ambapo Naibu waziri ameahidi kuyafanyia kazi kwa uzito maombi hayo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa