Katika kuadhimisha siku ya Lishe Kitaifa na Uzinduzi wa Kampeni ya Lishe kwa Vijana balehe Elimu imetolewa kwa Jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa kuzingatia ulaji wa makundi matano ya chakula kwa watoto kuanzia umri wa miezi sita hadi rika balehe itakayosaidia katika ukuaji wao na kuepuka magonjwa yasiyo ya lazima kama vile utapiamlo mkali na udumavu.
Maadhimisho hayo yamefanyika Oktoba 30, 2023 katika Ofisi ya Kijiji cha Ilonga Wilayani Kilosa ambapo mgeni rasmi akiwa Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Salome Mkinga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kilosa.
Amesema kuwa wazazi na walezi kwa ujumla ni jukumu lao kuzingatia na kuhakikisha watoto wanapata lishe bora ambayo itawafanya wakue vema na kuongeza utendaji kazi wa akili na uwezo wao kitaaluma samabamba na ubunifu wanapokuwa darasani.
Aidha Bi. Mkinga ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali inatekeleza Mwongozo wa Kitaifa wa utoaji huduma ya Chakula na Lishe shuleni ambao unalenga katika kuhakikisha kila mwanafunzi anapata angalau mlo mmoja akiwa shuleni na kuwajengea wanafunzi uelewa wanapokuwa katika masomo yao.
Naye Afisa Lishe wa Wilaya Bi. Zaina Kibona amewataka wazazi hasa wakiume kutoa ushirikiano wao katika kufatilia hatua za ukuaji wa watoto kwa kuzingatia lishe bora kwa ajili ya afya zao na kutowaachia akina mama peke yao.
Ameongeza kuwa juhudi mbalimbali zimeendelea kufanyika katika kuimarisha afya na ustawi wa vijana balehe kwa kuweka vipaumbele kwenye maeneo yanayolenga kutoa matokea chanya na ya haraka kwa vijana ikiwemo lishe.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Kijiji cha Ilonga Bi. Martha Kulewa ametoa wito kwa jamii juu ya upandaji wa bustani za mbogamboga kwa kutumia viroba ambapo haitaji eneo kubwa la shamba ili kurahisisha upatikani wa lishe bora kwa watoto kwa ajili ya ustawi wa afya zao na kuimarisha ukuaji na kuondoa udumavu na utapiamlo.
Maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa yanalenga kuimarisha Juhudi zilizopo nchini na yatajumuisha uzinduzi wa kampeni ya lishe kwa vijana balehe ambayo kauli mbiu ya maadhimisho 2023 “ Lishe bora kwa Vijana Balehe, Chachu ya Mafaniko yao”.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa