Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Abdallah Ulega amekiagiza Chuo cha Mifugo LITA Morogoro kuhakikisha kinawaleta wanachuo kwa mafunzo kwa vitendo katika maeneo husika hasa ya wafugaji badala ya kuwapeleka katika mafunzo kwa vitendo maeneo ya mijini yasiyo na jamii ya wafugaji kwani wakiwapeleka maeneo husika itasadia kuifanya kazi yao kwa vitendo lakini pia itawasaidia jamii husika hasa ya wafugaji kupata elimu namna ya kuandaa malisho ya mifugo yao.
Ulega amesema hayo alipokuwa katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Parakuyo ambapo amesema chuo hicho kinapasa kuwaleta wataalam katika maeneo ya ufugaji ili kuwasaidia wafugaji kuandaa namna bora ya kuandaa malisho kwa ajili ya mifugo hasa kipindi cha kiangazi kunapokuwa na uhaba wa malisho jambo ambalo husababisha wafugaji kuhama hama kwa ajili ya kutafuta malisho ambapo husababisha kutokea kwa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Naye mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amemshukuru Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa ziara yake ambapo ameagiza ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na meneja wa Lanchi ya Mkata kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa dhidi ya wawekezaji wasioendeleza maeneo wanayoyahodhi sambamba na wawekezaji waliokodisha maeneo ya lanchi kwa ajili ya kulima.
Aidha Mgoyi ametoa wito kwa wafugaji kuwa wakweli kuhusiana na idadi ya mifugo waliyonayo kwani kitendo cha kuwa wakweli kitasaidia wilaya kupanga mipango yake kwa usahihi na kwamba kwasasa baadhi ya wafugaji wameanza kuitumia vyema elimu ya ufugaji wa kisasa waliyopewa na kwamba ofisi yake inategemea wafugaji hao wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuijenga Kilosa Mpya.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilosa Ameir Mbarak amesisitiza kufanyika ka tahmini ya kina kutambua mipaka kwa maeneo ya wilaya ili kuepuka migogoro ya mipaka na uvamizi wa maeneo ama kutumika kwa maeneo kinyume na taratibu na kwamba kila mtu aheshimu maeneo hayo na kuyatumia kwa kufuata taratibu na sheria.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa