Mei 31 mwaka huu Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa pamoja na wafanyabiashara wilayani Kilosa wamepewa elimu ya utambuzi wa noti halali ikiwa ni tahadhari ya uwepo wa noti bandia zilizoko mitaani ambazo hazina thamani yoyote.
Elimu hiyo imetolea na Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutoka mkoani Dodoma Lilian Silaa ambapo amesema kuwa ni vema jamii ikafahamu kuwa kughushi ama kumiki fedha bandia kwa nia ya kuzitumia ni kosa la jinai ambapo yoyote atakayebainika atashtakiwa kwenye vyombo vya kisheria na endapo mtu akishuku uwepo wa noti bandia ni vema akaipeleka benki ama kituo cha polisi kwa uthibitisho.
Akieleza hatua za kutambua noti halalai amesema ni vema ukaichunguza fedha husika kwa umakini, fedha hiyo inapopapaswa ni lazima uhisi mparuzo kwenye maneno yaliyoandikwa kwa maandishi maalum, fedha hiyo pia itambulike kwa kuangalia sura ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inayoonekana unapoimulika noti kwenye mwanga pamoja na kutumia taa maalum yenye mwanga wa zambarau kuhakiki alama maalum zilizoonyeshwa kwenye vipeperushi na matangazo yanayohusu elimu ya fedha halali.
Aidha ameongeza kusema ni vema mwananchi au mtumiaji wa fedha akakagua utepe maalum kwenye noti ya shilingi 500/=, 2000/=, 5,000/= na 10,000/= unaoonekana kama madirisha yenye umbo la almasi ambao hubadilika badilika noti inapogeuzwa ambapo noti ya 1,000/= utepe wake ni tofauti.
Akihitimisha elimu hiyo Silaa ametoa wito kwa wananchi wenye noti zilizokatika kuzipeleka benki ambapo zitapokelewa na kwamba pesa zinazopokelewa ni zile zilizokatika na kutozidi vipande vinne huku akisisitiza watu kutouza fedha hizo kwa wajanja ambao huzinunua kwa kiwango pungufu ambapo wakishanunua huzipeleka benki na kupata fedha iliyokamilika na kupata faida huku muuzaji akipata hasara.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa