Kupitia kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani isemayo Familia na Jamii Tuwajibike Kuwatunza Wazee jamii na familia kiujumla imetakiwa kutambua kuwa wazee ni tunu kubwa katika maisha hivyo wanapaswa kutunzwa badala ya kunyanyaswa.
Wito huo umetolewa Oktoba 5 mwaka huu na Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Yohana Kasitila wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika kata ya Ruaha ambapo amesema wazee wanapaswa kutunzwa na kwamba Serikali inawathamini sana kwani wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali katika hali ya uzee.
Akibainisha namna Serikali inavyowajali amesema sera ya wazee ya mwaka 2003 lazima itazamwe kwa mapana yake na kutungiwa sheria ili wazee waweze kupata haki zao kama inavyostahiki ikiwemo uwepo wa dirisha la wazee litakalosimamia upatikanaji wa huduma za afya na huduma nyinginezo.
Pamoja na hayo Kasitila amesema upande wa Halmashauri maboresho ya upatikanaji wa huduma kwa wazee yanaendelea kwa kuhakikisha zahanati, vituo vya afya na hospitali kunakuwa na dirisha la wazee huku akiwashauri wazee hao kutumia vema fursa ya uwepo wa baraza la wazee kuainisha changamoto zao ili ziweze kushughulikiwa lakini pia kufanya mazoezi ya viungo ili kuwa na siha njema.
Akisoma risala ya wazee kwa niaba ya wazee wenzake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Leah Nzali amesema wazee ni kundi tete kutokana na hali zao kuwa duni kiafya na kiuchumi hivyo wanaomba kutazamwa kwa jicho la tatu huku wakiiomba Serikali ya awamu ya tano kuitazama sera ya wazee ambayo haijatungiwa sheria mchakato uweze kufanyika ili iweze kutekelezeka.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa