Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imekabidhi hundi ya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 110 kwa vikundi 12 ambayo ni mkopo kwa makundi ya Wanawake , Vijana na walemavu ikiwa ni asilimia kumi ya makusanyo ya mapato ya ndani kwa kipindi cha mwaka wa fedha mwezi Oktoba hadi Disemba 2019/2020 .
Hundi hiyo imekabidhiwa FebruarI 21 mwaka huu katika ukumbi wa halmashauri na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adamu Iddi mgoyi ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema kuwa anamshukuru Mkurugenzi na Halmashauri yake kwa ujumla kwa kufanya maamuzi magumu kutoa fedha za watu masikini na kutekeleza sheria ya Serikali kutoa asilimia kumi kwa makundi ya watu maalumu kwa asilimia mia moja.
MKUU WA WILAYA YA KILOSA ADAM MGOYI
Amesema kuwa Halmashauri kutoa fedha hizo si jambo jepesi kwasababu maagizo na maelekezo mengi ambayo Halmashauri wanayapata kutoka Serikali Kuu yanazidi asilimia miamoja ya mapato yote ya ndani na kwamba amevitaka vikundi vilivyo chukua fedha hizo wakatekeleze miradi walioombea mkopo na si vinginevyo, kwani fedha hiyo ni ya mkopo na inahitajika kurejeshwa kwa wakati ili watu wengine waweze kukopeshwa.
Mgoyi amesema vikundi hivyo lazima viwe na umiliki wa mradi kila mtu ashiriki na kufuatilia mwenendo wa mradi na sio kumuachia mtu mmoja kusimamia kwani ni muhimu kila mwana kikundi kushiriki katika vikao na kusomewa mapato na matumizi kwa mujibu wa taratibu zao za vikao na kwamba watambue kuwa Serikali ina mpango madhubuti wa kuwainua wananchi wake ili waondokane na umasikini hivyo fedha hizo hazitolewi kama zawadi bali zinatolewa kwa mkopo na kufanyiwa ufuatiliji ili ziweze kusaidia kuwaondoa katika umasikini kwani fedha hizo zikitumika kinyume na makusudio ya mkopo watapata hasara na kuishia pabaya.
KAIMU MKURUGENZI WA HALMASHAURI BW. NKELEGE (ALIYESIMAMA MWENYE SHATI LA KITENGE)
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa Cheyo Nkelege amesema kuwa Halmashauri imeweza kutenga asilimia 10 kwa makusanyo ya mapato ya ndani na kwamba Wilaya ya Kilosa ni kubwa na ina vikundi vingi, hivyo amewapongeza wale waliokidhi vigezo kupewa fedha hizo na kwamba amevitaka vikundi vikasimamie vizuri ili waweze kufikia malengo walio kusudia huku akiahidi kuwa Halmashauri itavifikia vikundi vyote vilivyo kidhi vigezo na kuvikopesha .
Akisoma taarifa ya kukabidhi hundi hiyo Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya Simforosa Mollel amesema kuwa Halmashauri imeendelea kutekeleza takwa la kisheria la kutoa mikopo ya makundi maalumu ambapo katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2019/2020 Halmashauri imeweza kutoa fedha kwa mifuko ya maendeleo ya wanawake ,Vijana na watu wenye ulemavu kiasi cha shilingi milioni mia moja na kumi , lakitano ishirini na tisa ,mia mbili ishirini na tisa senti sita tisa(110,529,226.69) zimeidhinishwa kutolewa ili walengwa wenye sifa waweze kupata mikopo hiyo kama ilivyoainishwa katika sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 na marekebisho yake ya mwaka 2018 huku akisema kuwa jumla ya vikundi kumi na mbili [12] vimeidhinishiwa mkopo ambapo vikundi vya wanawake vimepata kiasi cha shilingi milioni 44,211690.68, vijana 44,211690.68 na watu wenye ulemavu Tsh 22 105845.33.
MAKAMU MWENYEKITI WA HALMASHAURI MH. HASSAN KAMBENGA AKIWA NI MOJA KATI YA WALIOSHUHUDIA ZOEZI HILO LA KUKABIDHI HUNDI
Nao wana vikundi wameishukuru Halmashauri kwa ujumla kwa kuwaamini kwani jamii imekuwa na mtazamo hasi kwa vijana kuwa hawaaminiki na kwamba wameihakikishia Halmashauri kuwa fedha waliyokopeshwa itakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa na kuzirejesha kwa muda muafaka ili ziweze kusaidia na wengine.
BAADHI YA WANAVIKUNDI WALIOKABIDHIWA MKOPO NA HALMASHAURI YA WILAYA YA KILOSA
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa